August 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TanTrade yasisitiza utafiti masoko kuongeza Kilimo


Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeeleza kuwa inaendelea kufanya tafiti za masoko ili kubaini mahitaji, viwango vya ubora na gharama halisi zinazohusika katika mnyororo mzima wa thamani, hatua inayolenga kuwawezesha wazalishaji wa ndani kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Ephraim Balozi Mafuru, alisema tafiti hizo ni sehemu ya mikakati ya Mamlaka hiyo ya kuhakikisha wazalishaji wanapata taarifa sahihi kuhusu masoko kabla ya kuzalisha, badala ya kuzalisha bila kuzingatia mahitaji ya walaji.


Alisema TanTrade inaendelea kutafuta na kuchambua masoko ili kubaini mahitaji yake, ubora unaohitajika pamoja na gharama zinazojitokeza katika hatua mbalimbali za mnyororo wa thamani, kisha kutumia taarifa hizo kuwawezesha na kuwahamasisha wazalishaji wa ndani kuongeza uzalishaji wenye tija.


“TanTrade inaendelea kufanya utafiti wa masoko, kutambua mahitaji ya soko, kujua ubora unaohitajika na gharama halisi zinazohusika katika mnyororo mzima wa thamani, kisha kuwawezesha wazalishaji wa ndani,” alisema Mafuru.


Kauli hiyo inaendana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya TanTrade na Wizara ya Kilimo ya kuimarisha ushirikiano katika kutafuta na kuunganisha masoko ya ndani, kikanda na kimataifa kwa ajili ya mazao ya kilimo.


Makubaliano hayo yalifikiwa katika mazungumzo kati ya Mafuru na Waziri wa Kilimo, Daniel Godfrey Chongolo, yaliyofanyika mara baada ya kilele cha Maonesho ya Nane Nane 2026 jijini Dodoma.


Kwa mujibu wa makubaliano hayo, ushirikiano huo utajikita katika matumizi ya taarifa za masoko, utafutaji wa masoko mapya, uongezaji thamani wa mazao na kukuza biashara ya mazao ya kimkakati, yakiwemo zabibu, asali na mazao yanayotumika kuzalisha mafuta ya kula.


Mafuru alisema matumizi ya taarifa sahihi za masoko ni muhimu katika kubadili namna ya uzalishaji nchini, kwa kuhakikisha wazalishaji wanaelekeza nguvu zao katika bidhaa ambazo zina mahitaji na fursa katika masoko mbalimbali.

Alisema hatua hiyo pia inalenga kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini, kuwaongezea wazalishaji fursa za kupata masoko na hatimaye kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kabla hayajafikishwa kwa walaji.


Ushirikiano kati ya TanTrade na Wizara ya Kilimo unatarajiwa pia kusaidia kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya kimkakati kwa kuunganisha uzalishaji, uchakataji, uongezaji thamani na masoko.


Kwa kufanya hivyo, taasisi hizo zinalenga kuhakikisha uzalishaji wa mazao unaongozwa zaidi na mahitaji ya soko, badala ya kutegemea uzalishaji pekee bila kuwa na uhakika wa soko la bidhaa husika.


Alisema ,hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kukuza biashara ya mazao ya kilimo, kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa taifa, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.