August 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waandaaji wa maonesho watakiwa kufuata taratibu

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imewataka waandaaji wa maonesho, makongamano, misafara ya kibiashara na matukio ya ukuzaji biashara kuhakikisha wanapata vibali kutoka mamlaka hiyo kabla ya kuendesha shughuli hizo, ili kuepusha migogoro na changamoto zinazoweza kujitokeza kati ya waandaaji na washiriki.

Wito huo umetolewa Agosti 8,2026 na Msimamizi wa Ofisi ya TanTrade Kanda ya Ziwa,Ofisa Mwandamizi wa mamlaka hiyo Cecilia Mwandepa,wakati akieleza huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo katika kilele cha maonesho ya Nanenane,ambayo kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yamefanyika katika viwanja vya Nyamh’ongolo wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Ambapo amesema,kwa mujibu wa sheria, TanTrade ina dhamana ya kutoa vibali kwa watu binafsi au taasisi zinazoandaa maonesho ya biashara ya ndani na nje ya nchi, makongamano na misafara ya kibiashara.

Mwandepa amesema,mbali na kutoa vibali,TanTrade pia utoa ushauri wa kitaalamu kwa waandaaji wa matukio hayo kuhusu namna bora ya kuyaandaa na kuyatekeleza kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Amesema,kumekuwa na wimbi kubwa la kampuni na taasisi kuandaa matukio ya ukuzaji biashara bila kufuata utaratibu, jambo ambalo linaweza kusababisha changamoto mbalimbali ikiwemo wizi na migogoro kati ya waandaaji na washiriki.

“Mara nyingi zikitokea kesi kama hizo zinaletwa TanTrade kutatuliwa,ndiyo maana tunawahamasisha kabla hujaandaa maonesho yako ya ukuzaji biashara ufike katika mamlaka hii,ili upewe utaratibu wa kuandaa tukio hilo pamoja na kupatiwa kibali, ili kuonesha kuwa wewe ni mwandaaji rasmi wa tukio hilo,”amesema Mwandepa.

Amesisitiza kuwa iwapo tukio litaandaliwa bila kibali, TanTrade hutoa tangazo kuwa tukio hilo halina kibali wala idhini ya mamlaka hiyo na kwamba haitahusika na lolote litakalotokea.

Sanjari na hayo amesema,TanTrade imeshirik katika maonesho ya Nanenane kwa kutoa huduma mbalimbali, ikiwemo taarifa za biashara,kufanya tafiti na kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu namna ya kuboresha bidhaa zao ili zikidhi vigezo vya masoko ya ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo amesema,mamlaka hiyo pia ina jukumu la kukuza chapa za bidhaa za Tanzania, ambapo mwaka jana ilizindua nembo ya Taifa inayojulikana kama “Made in Tanzania”, inayowekwa kwenye bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kwa lengo la kuzitambulisha katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mwandepa amewataka,Watanzania, hususani wafanyabiashara na wazalishaji, kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa hapa nchini zinakuwa na nembo hiyo,ambapo amesema inasaidia bidhaa kutambulika,kupata masoko endelevu na kujenga uzalendo.

Kwa upande wa Kanda ya Ziwa amesema,wameanza kuhamasisha matumizi ya nembo ya “Made in Tanzania”, kupitia maonesho ya Nanenane, ambapo mwitikio umekuwa mkubwa na chanya.

Huku baadhi ya wazalishaji walionesha kutokuwa na uelewa kuhusu nembo hiyo, hivyo walipewa elimu na kusisitizwa kuhakikisha bidhaa wanazozalisha hapa nchini zinakuwa na nembo hiyo.