August 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima zaidi ya 200 wapatiwa elimu matumizi ya viuatilifu

Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline,Arusha

WAKULIMA zaidi ya 200 wamepatiwa elimu kuhusu matumizi sahihi na salama ya viuatilifu katika mazao yao ili kuweza kujiepusha na madhara yatokanayo na upuliziaji wa simu kwenye mazao kienyeji

Akizungumza na wakulima Agosti 7,2026 kwenye maonesho ya nane nane Arusha,Afisa Kilimo Msaidizi kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viwatilifu (TPHPA), Ramadhani Masele, amesema elimu hiyo inalenga kuboresha afya na usalama wa wakulima pamoja na walaji, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu bora za matumizi ya viuatilifu .

Amesema wakulima wanapaswa kuvaa vifaa maalumu vya kujikinga wanapokuwa wakichanganya au kunyunyizia viwatilifu kwenye mazao, ili kulinda afya zao dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza.

Aidha, amewataka wakulima kusoma kwa umakini maelekezo yaliyo kwenye vifungashio vya viwatilifu kabla ya kuvitumia, ikiwemo kuzingatia muda sahihi wa kusubiri baada ya kunyunyizia dawa kabla ya kuvuna au kutumia mazao kwa chakula.

Masele ameeleza kuwa matumizi ya mazao mara baada ya kunyunyiziwa viuatilifu bila kuzingatia muda uliowekwa yanaweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu, yakiwemo matatizo ya mfumo wa chakula na madhara kwa viungo vya mwili.

Ametoa wito kwa wakulima kuendelea kutembelea Mamlaka hiyo ili kupata elimu zaidi kuhusu matumizi salama na sahihi ya viuatilifu , pamoja na namna bora ya kulinda afya zao na za walaji.
Katika maonesho hayo, TPHPA pia imeendelea kuwaelimisha wakulima kuhusu teknolojia mpya za vifaa vya kunyunyizia viwatilifu, ikiwemo mabomba ya kunyunyizia dawa yanayoweza kuchajiwa na kutumika mashambani.