Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Ziwa, imetoa onyo kwa wanaotoa huduma au kufanya biashara zilizopo chini ya udhibiti wake bila kuwa na leseni, huku ikitaja kuwa faini yake ni kubwa na inaanzia shilingi milioni 3 hadi milioni 20 kwa mujibu wa sheria.
Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Nyirabu Musira,akizungumza na waandishi wa habari Agosti 7,2026, walipotembelea banda la mamlaka hiyo kwenye maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi, yanayofanyika katika Viwanja vya Nyamhongolo, Wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Musira amesema,katika kipindi chote cha maonesho hayo, ofisi ya kanda imekuwa na wakati mzuri wa kupokea wananchi wengi ambao wamewapatia elimu kuhusu sekta inayosimamia na shughuli za mamlaka hiyo,namna ya kupata leseni za ujenzi wa miundombinu ya vituo vya mafuta na mifumo ya umeme.
Amesma, kupitia maonesho hayo EWURA imeweka msisitizo kwa wananchi kuhakikisha wanatumia mafundi umeme wenye leseni kutoka mamlaka hiyo na kuepuka “vishoka”, kwani kundi hilo husababisha uharibifu au ajali za moto kwenye majengo, hali inayowasababishia wahusika kukosa fidia pindi majanga yanapotokea.
“Rai yetu kwa umma ni kuhakikisha wanajiridhisha kama watoa huduma wetu wana leseni. Kwenye nishati tunadhibiti petroli, gesi asilia, na umeme.Unapotaka kujenga nyumba na kuweka mifumo ya umeme, au unapotaka kununua mafuta na gesi ya kupikia, hakikisha unanunua kwa mtu mwenye leseni halali ya EWURA,” alisisitiza Musira.
Hata hivyo amefafanua namna mwananchi anavyoweza kumtambua mtoa huduma halali,ambapo amesema, kuwa leseni za mafundi wanaofunga mifumo ya umeme ni ndogo kama leseni za udereva na wanapaswa kutembea nazo wakati wote, hivyo mwananchi ana haki ya kuziomba na kuzikagua huku kwa wafanyabiashara wa vituo au maduka, wanatakiwa kuzining’aniza leseni zao wazi maeneo ya biashara.
“Mtu mwenye leseni ya EWURA utamjua tu kwa jinsi anavyofuata utaratibu. Mfano, ukienda kununua gesi kwa mtu asiye na leseni, huwezi kukuta mizani ya kupimia,lakini mwenye leseni ana mizani, na mitungi yake imefunikwa vizuri (seal),”amesema Musira.
Kuhusu athari za kutumia huduma zisizodhibitiwa,Musira ametahadharisha kuwa jambo hilo linahatarisha usalama wa raia,mali na mazingira,ametolea mfano mitungi ya gesi inayouzwa kiholela kuwa inaweza kuwa haijahakikiwa na inavuja hivyo kusababisha milipuko, au ikawa na uzito pungufu unaompa mnunuzi hasara.
Aidha, Musira amesema,EWURA imetumia maonesho hayo kuhimiza umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku wakipokea maoni na malalamiko ya wananchi kuhusu gharama za gesi ya nyumbani pamoja na maswali ya lini gesi asilia itafika katika maeneo yao.

More Stories
Mamlaka ya maji Mbeya yaonya wanaoiba mifuniko
Busokelo yajipanga kumaliza udumavu
UDOM yajidhatiti katika bunifu kutatua changamoto za jamii