Na Joyce Kasiki, Dodoma
MJASIRIAMALI wa bidhaa za nyuki, Noreen Banyema maarufu Bee Blessing, amesema uongezaji thamani wa mazao ya nyuki umefungua fursa za ajira na biashara kwa vijana, huku ongezeko la matumizi ya bidhaa za asali likichochewa na kuimarika kwa uelewa wa wananchi kuhusu faida zake kiafya.
Banyema alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika Maonesho ya Nanenane 2026 kupitia Programu ya Building a Better Tomorrow (BBT) chini ya Wizara ya Kilimo. Alisema kupitia shughuli zake ameweza kujiajiri, kuajiri vijana watatu wa kudumu na wawili wa muda, sambamba na kupanua masoko ya bidhaa zake ndani na nje ya nchi.
Alisema anajishughulisha na uzalishaji, ununuzi na uongezaji thamani wa mazao ya nyuki kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zenye ubora wa hali ya juu ili kukidhi mahitaji ya soko.
Kwa mujibu wake, bidhaa anazozalisha ni pamoja na asali ya nyuki wadogo, asali ya nyuki wakubwa, chavua ya nyuki (bee pollen), maziwa ya nyuki (royal jelly), asali ya viungo, tangawizilishi na bidhaa ya mixed nuts inayochanganya karanga, korosho, almond na mbegu za maboga zilizoongezwa asali mbichi pamoja na bee pollen.
Alieleza kuwa asali ya viungo hutengenezwa kwa kutumia tangawizi, karafuu na mdalasini vinavyolimwa nchini, hatua inayoongeza thamani ya mazao ya wakulima na kuzalisha bidhaa yenye virutubisho vingi inayotumika kama kiongozea cha chai na kwa matumizi ya kiafya.
Aidha, alisema mazao ya nyuki hayatumiki kwa chakula pekee bali pia ni malighafi katika utengenezaji wa sabuni, mafuta na bidhaa nyingine za urembo, jambo linaloongeza fursa za biashara katika sekta hiyo.
Alisema mahitaji ya bidhaa za nyuki yameendelea kuongezeka kadri wananchi wanavyozidi kuelewa umuhimu wa asali na mazao mengine ya nyuki, huku wengi wakipunguza matumizi ya sukari na kutumia asali asilia kama mbadala.
Aliongeza kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii yamekuwa nyenzo muhimu ya kutangaza bidhaa zake na kuwafikia wateja wengi zaidi ndani na nje ya Tanzania.
Mjasiriamali huyo aliishukuru Serikali kwa kuanzisha Programu ya BBT, akisema imewapa vijana fursa ya kushiriki Maonesho ya Nanenane, kutangaza biashara zao, kujifunza kutoka kwa wadau mbalimbali na kujenga mitandao ya kibiashara.
Aliwataka vijana kutumia fursa zilizopo katika kilimo, ufugaji na uongezaji thamani wa mazao badala ya kusubiri ajira rasmi, akisisitiza umuhimu wa kujifunza, kuuliza maswali, kutumia mitandao ya kijamii na kufuatilia taarifa za fursa kutoka taasisi mbalimbali.
Pia aliiomba Serikali kuendelea kuwekeza katika sekta ya nyuki na kuweka mazingira rafiki kwa wajasiriamali ili kuongeza uzalishaji, ajira na mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

More Stories
T-CAMS yaleta mapinduzi sekta ya uwakala wa forodha
Mafuta ya zabibu yavutia Nanenane
Nanauka apongeza Kariakoo Kwa kuwezesha vijana Kibiashara