August 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wachimbaji wadogo Namungo waomba mafunzo endelevu ya usalama na afya kazini

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

Wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Namungo wameiomba Serikali kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuwapatia mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi mara kwa mara ili waweze kutekeleza shughuli za uchimbaji na uchakataji madini kwa kuzingatia kanuni bora za usalama na afya mahali pa kazi.

Wamewasilisha maombi hayo baada ya kushiriki mafunzo ya usalama na afya yaliyoandaliwa na OSHA kwa wachimbaji wadogo zaidi ya 400 wanaofanya shughuli zao katika Mgodi wa Namungo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakiwemo Ramadhan Abdallah na Salum Mfaume wamesema wamejifunza mambo mengi muhimu kupitia mafunzo hayo yaliyotolewa kwao Agosti 4, 2026 ambapo wamesisitiza kwamba mafunzo hayo yatabadilisha utamaduni wa kutozingatia tahadhari katika shughuli zao za kila siku.

“Kwasiku ya leo tunashukuru ujio wa OSHA ambao wametupa elimu ambayo itatusaidia sana katika shughuli zetu za kila siku lakini pia elimu ambayo tunatakiwa kuendelea kuizingatia ili iweze kutuletea manufaa. Tunawashukuru sana na pia tunawaomba muendelee kutupatia mafunzo haya mara kwa mara,” amesema Ramadhani Abdallah.

“Binafsi nawashukuru OSHA kwa kuja kututembelea leo, kifupi tumejifunza mambo mengi sana kupitia wao hivyo tunaomba isiwe mwisho leo na tunaomba utaratibu huu uwe endelevu katika vipindi tofauti tofauti,” ameeleza Salum Mfaume.

Akisoma risala ya wachimbaji hao mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, Katibu wa Chama cha Wachimbaji Namungo, Bw. Emmanuel Johanes amesema wamepata mafanikio makubwa katika shughuli za uchimbaji madini kutokana na ushirikiano uliopo baina yao na Taasisi za serikali ikiwemo OSHA.

“Kampuni ya Elianje Genisis inayomiliki leseni ya eneo hili tunalofanya shughuli zetu za uchimbaji imefanya maboresho makubwa sana katika miundombinu ya uchimbaji kwa kuweka kiupaumbele katika usalama, afya na ulinzi wa wafanyakazi. Maboresho hayo yemefanyika kwa ushirikiano na Taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo OSHA. Hatua hii imetokana na imani yetu kwamba maisha ya wafanyakazi yana thamani kubwa kuliko uzalishaji wowote unaoweza kufanyika,” ameeleza Bw. Emmanuel Johanes.

Akiwahutubia washiriki wa mafunzo hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, amesema mafunzo ya usalama na afya ni muhimu ili kuwawezesha wachimbaji kuchukua tahadhari dhidi vihatarishi vingi vilivyopo katika shughuli za uchimbaji madini.

Aidha, amebainisha kwamba mafunzo hayo yametolewa kwa muda mfupi hivyo hayawezi kukidhi mahitaji ya elimu ya usalama na afya kwa wachimbaji hao ambapo ameahidi kumwelekeza Mtendaji Mkuu wa OSHA kuandaa mafunzo zaidi kwa ajili ya kundi hilo lenye wachimbaji wadogo zaidi ya 4,000.

Mgodi wa Namungo unamilikiwa na Kampuni ya Elianje Genesis ambayo imetoa nafasi kwa wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao ndani ya mgodi huo na kuuza madini kwa kampuni hiyo. Madini yanayopatikana katika mgodi huo ni pamoja na dhahabu, green garnet pamoja na grahite.