August 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ummy atangaza fursa banda la Ofisi ya Waziri Mkuu


Na Joyce Kasiki,Dodoma

NAIBU Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Watu Wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga, amewahimiza Watanzania kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu katika maonesho yanayoendelea ili kupata huduma mbalimbali, elimu na fursa zinazotolewa na taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Nderiananga alisema ameridhishwa na maandalizi yaliyofanywa na watumishi pamoja na ushiriki wa taasisi mbalimbali zinazotoa huduma kwa wananchi.
Alisema  kuwa wageni watapata nafasi ya kutatuliwa changamoto zao papo hapo au kuunganishwa na sekta husika kwa ajili ya huduma zaidi.

Aidha, alimpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Profesa Palamagamba Kabudi, kwa uongozi wake, pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deus Sangu, kwa usimamizi wa majukumu katika sekta zao. Pia alimshukuru Waziri Mkuu kwa uratibu na uongozi unaowezesha utekelezaji wa majukumu ya wizara hizo.

Nderiananga alisema banda hilo limekusanya taasisi mbalimbali ikiwemo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PSSSF, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), programu za maendeleo ya kilimo zinazofadhiliwa na IFAD, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Mamlaka ya Dawa za Kulevya (DCEA) pamoja na kitengo cha watu wenye ulemavu kinachotoa elimu na huduma kwa wananchi.

Alieleza kuwa uwepo wa taasisi hizo sehemu moja unarahisisha wananchi kupata huduma mbalimbali kwa wakati mmoja na kuongeza uelewa kuhusu mipango na programu zinazotekelezwa na Serikali.

Amewakaribisha wananchi kuendelea kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu ili kujionea kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.