Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dodoma
MKULIMA na mnunuaji mkubwa wa mpunga kutoka kwa wakulima wenzake Kanda ya Ziwa, Adam Horoma ameeleza mafanikio yake yametokana baada ya kukopeshwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).
Amesema hayo leo Agosti 6, 2026 kwa waandishi wa habari, mara baada ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Hamad Hassan Chande kupita kwenye Kizimba chake kilichopo Banda la Benki ya TADB kwenye Maonesho ya Kilimo (Nanenane) katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma.

Horoma ambaye anatoka Kagongwa, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, amesema, pamoja na kulima, pia ananunua mazao kutoka kwa wakulima wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, sababu amejenga kiwanda ambacho kinamsaidia kuweza kukoboa mpunga huo na kuweza kuuza ndani na nje ya nchi.
“Pamoja na kulima, pia tunanunua mpunga kwa wakulima waliopo Mkoa wa Shinyaga na Kanda ya Ziwa yote. Zaidi ya gunia milioni moja tunanunua kwa msimu mmoja, hivyo kufanya hata wakulima kutegemea kiwanda changu cha Horoma Rice Mill Ltd kwenye ununuzi wa mazao yao ya mpunga” amesema Horoma.
Awali, akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Hamad Hassan Chande, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TADB, Yodas Mwanakatwe amesema katika kuhakikisha Tanzania ina utoshelevu wa mazao ya chakula na biashara, imekuwa ikiwasaidia wakulima kwa kutoa mikopo ili kuwawezesha kulima mazao ambayo watauza ndani na nje ya nchi.

Mwanakatwe amesema mkulima kutoka Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga Adam Horoma, ambaye yupo kwenye Banda la Nanenane la TADB, amewezeshwa na benki hiyo kwa kupewa mkopo, na mchele wake ambao una ubora, anauza ndani na nje ya nchi.
“Kama TADB, tuna jukumu la kuhakikisha nchi ina utoshelevu wa chakula, kwa hiyo tumewekeza sana pia kwenye mazao ya chakula, huyu (Horoma) ni mmoja wa wanufaika wetu anbaye ametokea Kahama. Ukitaka kupata mchele mzuri, moja ya maeneo yanatoa mchele mzuri ni Kahama. Bahati nzuri bidhaa zake ameziweka kwenye ubora wa kuhudumia soko la ndani na nje ya nchi” amesema Mwanakatwe.

Mwanakatwe amesema wanasaidia sana mazao mengine kuona yanafanya vizuri ndani na nje ya nchi, na kwenye banda lao wamewakaribisha wakulima wa korosho, zabibu, alizeti, watengeneza mvinyo wa zabibu, watengeneza bidhaa za mbolea za asili (samadi) na kahawa, ambao wote hao wanaungwa mkono na Benki ya TADB kwa kupewa mikopo.
“Tupo na wadau wetu watatu, Karagwe District Co- coparative Union Ltd kutokea Karagwe, Mbozi Cofee Company Ltd, na Mambo Roasted kutoka Morogoro. Pia tuna wanufaika wengine, huyu ni Keen Feeders ambaye anazalisha pembejeo ambayo ipo kwenye mbolea. na huyu anatokea Arusha. Pia tuna mdau mwingine Almah Agro Group, na hiki ni kiwanda kipya kabisa hapa Dodoma yeye anazalisha mbolea ya samadi.

“Lakini Kanda ya Kati tumebarikiwa kuwa na mazao ya misitu ikiwemo asali. Hii ni asali yenye ubora, na masoko yake mengi yapo nje ya nchi, na huyu yupo hapa hapa Dodoma, na bidhaa zake nyingine zipo Super Market. Lakini pia tuna mkulima mwingine wa asali kutoka Dodoma, hivyo tunapowainua hawa wazalishaji wa bidhaa hizi, manufaa yanarudi kwa mkulima”amesema Mwanakatwe.
Naibu Waziri, Chande alitoa ushauri kwa TADB kwa kufanyia utafiti matunda ya korosho maarufu kama mabibo, kwani hayo yakitumika vizuri yanaweza kutengeneza Mvinyo (Wine).





More Stories
Dkt Chaya:Tagazeni mafanikio ya Kampeni ya mama Samia legal Aid
FAO yawataka wakulima kuzingatia kanuni bora za ufugaji
TanTrade kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania,Serbia