Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Shirika lisilo la kiserikali la Msichana Initiative limewapa mafunzo waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo wa kutumia taaluma yao kuelimisha jamii na kuhamasisha mapambano dhidi ya ndoa za utotoni, ambazo zinaendelea kuwanyima maelfu ya watoto wa kike haki ya elimu na kutimiza ndoto zao.
Mafunzo hayo yalijikita katika Communications and Advocacy Strategy ya Msichana Initiative, yakilenga kuwapa waandishi mbinu za kuandaa habari zenye kuchochea mabadiliko ya kijamii na kuimarisha utetezi wa haki za mtoto wa kike.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Initiative, Consolata Chikoti, amesema licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo, ndoa za utotoni bado zinaendelea kufanyika kwa siri katika baadhi ya maeneo ya vijijini.
Amesema hali hiyo inachangiwa na mila potofu pamoja na tamaa ya mahari, ambapo baadhi ya watoto wa kike huondolewa shuleni na kulazimishwa kuolewa bila ridhaa yao, jambo linalowanyima fursa ya elimu na kuongeza mzunguko wa umaskini katika jamii.
“Kupitia vyombo vya habari tunaamini mna nafasi kubwa ya kushirikiana nasi kuendeleza ajenda ya haki, usawa na uwezeshaji wa mtoto wa kike. Tunahitaji kuona taarifa zinazoripotiwa zikichochea mabadiliko chanya katika jamii na kusaidia kutokomeza ndoa za utotoni,” amesema Chikoti.

Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo kuhusu mawasiliano na utetezi, Francis Shao, amesema vita dhidi ya ndoa za utotoni haviwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, vyombo vya habari, asasi za kiraia na wadau wengine wa maendeleo.
Amesisitiza kuwa waandishi wa habari wana nafasi muhimu ya kuelimisha umma, kufichua vitendo vinavyokiuka haki za watoto na kuhamasisha jamii kulinda na kutetea haki za mtoto wa kike.

Naye mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, Jakobo Mosenda, ameipongeza Msichana Initiative kwa kuandaa mafunzo hayo, akisema yameongeza uelewa wake kuhusu namna ya kuandaa habari zenye kuhamasisha jamii kupinga ndoa za utotoni na kutetea haki za wasichana kupata elimu na fursa za maendeleo.

Amesema maarifa aliyopata yatamwezesha kuandika habari zenye athari chanya kwa jamii, kuongeza uelewa kuhusu madhara ya ndoa za utotoni na kuchangia katika juhudi za kuhakikisha kila mtoto wa kike anapata nafasi ya kutimiza ndoto zake.

More Stories
Mbolea ya fomi yaleta neema kwa wakulima
Takwimu sahihi zatajwa nguzo muhimu maendeleo ya Taifa
SELF yawahamasisha wananchi kutumia fursa za mikopo