Na Joyce Kasiki, Dodoma
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imewataka wananchi, wawekezaji na wadau mbalimbali kushirikiana na taasisi hiyo katika utoaji wa taarifa sahihi ili kuwezesha uzalishaji wa takwimu rasmi zenye ubora zinazosaidia kupanga, kutekeleza na kutathmini mipango ya maendeleo ya Taifa.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa NBS, Ruth Minja, alipokuwa akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Alisema ushiriki wa NBS katika maonesho hayo unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi, kutoa elimu kuhusu matumizi ya takwimu rasmi na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika tafiti mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo.
Minja alisema, kwa mujibu wa sheria, NBS ina jukumu la kuzalisha na kuratibu takwimu rasmi nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, ajira, usafirishaji, mwenendo wa bei, mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema takwimu hizo ni msingi wa uandaaji wa sera, mipango ya maendeleo na tathmini ya utekelezaji wake.
“Takwimu tunazozalisha ndizo msingi wa maamuzi sahihi. Zinasaidia kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kupima hatua za kufikia malengo ya Taifa,” alisema Minja.
Alieleza kuwa takwimu za kilimo huwasaidia wakulima, wafanyabiashara na wawekezaji kutambua maeneo ya uzalishaji, kiwango cha mazao na fursa zilizopo kwenye masoko.
Aidha, alisema takwimu za idadi ya watu husaidia kutambua ukubwa wa soko, mahitaji ya wananchi na maeneo yenye fursa za uwekezaji.
Minja alisema NBS hukusanya taarifa kupitia sensa na tafiti mbalimbali za kaya, taasisi na sekta tofauti, huku akisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi katika kutoa taarifa sahihi ndio msingi wa kupata takwimu zenye uhakika.
Aliwataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika tafiti zote zinazoratibiwa na NBS ili kuiwezesha nchi kuwa na takwimu zitakazochochea maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.
Wakati huo huo, Kaimu Meneja wa Takwimu za Kilimo wa NBS, Philemon Mwenda, alisema takwimu za kilimo hazihusu uzalishaji wa mazao pekee, bali pia zinajumuisha sekta za mifugo, uvuvi, misitu na mazao yake.
Alisema mtazamo huo unatoa picha kamili ya mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa Taifa na kuwezesha maamuzi sahihi ya kisera na kiuwekezaji.
“Tunapozungumzia takwimu za kilimo hatumaanishi mazao pekee. Tunahusisha pia mifugo, uvuvi, misitu na mazao yake kwa kuwa zote ni sehemu ya sekta ya kilimo,” alisema Mwenda.
Aliongeza kuwa tafiti za NBS zinaonesha kuwa nafaka zimeendelea kuwa chakula kinachotumiwa zaidi na Watanzania kwa miaka kadhaa, huku mahindi na mchele vikiongoza katika matumizi ya kila siku.
Kwa mujibu wa Mwenda, takwimu hizo zinaonesha pia kuwa tofauti ya matumizi ya nafaka kati ya mikoa mbalimbali ni ndogo, jambo linaloakisi kufanana kwa utamaduni wa ulaji miongoni mwa Watanzania.

More Stories
Mbolea ya fomi yaleta neema kwa wakulima
Msichana Initiative yawajengea uwezo Waandishi wa habari kupinga ndoa za Utotoni
SELF yawahamasisha wananchi kutumia fursa za mikopo