August 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Teknolojia mpya yainua tija zao la Pamba Tanzania


Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

BODI ya Pamba Tanzania (TCB) imeendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia mpya katika kilimo cha pamba kwa lengo la kuongeza uzalishaji, kuinua kipato cha wakulima na kuongeza thamani ya zao hilo kupitia uchakataji wa bidhaa mbalimbali.


Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi na Uthibiti kutoka Bodi ya Pamba Tanzania, James Shimbe, alisema hayo wakati wa Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, akieleza kuwa sekta hiyo imeendelea kuboreshwa kuanzia uzalishaji wa shambani hadi hatua za uchakataji.


Alisema moja ya hatua kubwa zilizochukuliwa ni kuanzishwa kwa mfumo mpya wa upandaji wa pamba unaolenga kuongeza idadi ya mimea kwa ekari na hivyo kuongeza kiwango cha mavuno kwa wakulima.


“Kwa kutumia teknolojia hii, idadi ya mimea kwa ekari imeongezeka kutoka wastani wa miche 22,000 iliyokuwa ikitumika awali hadi kufikia miche 44,000. Ongezeko hilo linaongeza msongamano wa mimea na kutoa nafasi ya kuongeza uzalishaji,” alisema.


Shimbe alisema kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo, wakulima wanaweza kuvuna kati ya kilo 500 hadi zaidi ya kilo 1,000 kwa ekari, huku baadhi wakifikia kilo 2,000, tofauti na zamani ambapo wengi walikuwa wakipata wastani wa kilo 250 hadi 300 kwa ekari.


Aidha, alisema Bodi imeboresha matumizi ya mbegu za pamba kwa kuanzisha mbegu bora zilizoboreshwa kwa kuondolewa nyuzi (linters), ambazo zimeongeza uwezo wa kuota hadi zaidi ya asilimia 90 na hivyo kusaidia wakulima kupata mimea yenye afya na mavuno bora.


Alieleza kuwa pamoja na kuongeza uzalishaji, Bodi inaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuongeza thamani ya zao la pamba kupitia uchakataji ili kuhakikisha manufaa ya zao hilo yanaonekana katika mnyororo mzima wa thamani.


“Pamba siyo tu nyuzi zinazouzwa nje, bali inaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vitambaa, mashati, vitenge, mashuka na bidhaa nyingine za nguo zinazoongeza ajira na mapato,” alisema.


Aliongeza kuwa mbegu za pamba nazo zina mchango mkubwa kiuchumi baada ya kuchakatwa, ambapo huzalisha mafuta ya kula kwa matumizi ya binadamu pamoja na mashudu yanayotumika kama chakula cha mifugo.


Hata hivyo, Shimbe alisema sekta ya pamba bado inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo utegemezi mkubwa wa mvua, kutokana na zao hilo kulimwa kwa kutegemea mvua kwa asilimia 100.


Alisema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa na athari katika uzalishaji pale mvua inapokuwa haitabiriki, hali inayoweza kupunguza mavuno, huku misimu yenye mvua nzuri ikiwezesha wakulima kupata uzalishaji mkubwa na kipato kizuri.


Katika upande wa masoko, alisema mabadiliko ya bei ya pamba katika soko la dunia ni changamoto nyingine inayoathiri bei ya zao hilo nchini kutokana na mfumo wa soko huria.


Alisema bei inapokuwa nzuri huongeza hamasa kwa wakulima kuzalisha zaidi, lakini inaposhuka baadhi yao huamua kuelekeza nguvu kwenye mazao mengine yenye uhakika wa kipato.


Pamoja na changamoto hizo, Shimbe alisema kipaumbele cha Bodi ya Pamba Tanzania ni kuongeza uzalishaji wenye tija kwa kuwahimiza wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo, ikiwemo kuandaa mashamba mapema, kutumia mbegu bora na kutunza mazingira.


Aidha, alisema Bodi imeanza kuhamasisha matumizi ya mabaki ya pamba kutengeneza mbolea ya asili kwa kutumia teknolojia iliyopatikana kutoka Brazil, hatua inayolenga kurejesha rutuba ya udongo na kuendeleza uzalishaji endelevu wa zao hilo nchini.