Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
SHIRIKA la INADES Formation Tanzania (IFTz) limesema linaendelea kuwawezesha wakulima, wafugaji na wananchi kwa ujumla kuongeza tija katika uzalishaji kupitia matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, kuongeza thamani ya mazao na kuwaunganisha na fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa IFTz, Jacqueline Nicodemus, alisema shirika hilo limejikita katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kushirikiana na Serikali, sekta binafsi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Alisema ushiriki wa IFTz katika maonesho hayo unaendana na kaulimbiu ya mwaka ya “Tambua Soko, Ongeza Tija”, kwa kutoa elimu inayowasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kuunganisha bidhaa zao na masoko yenye uhakika.
Nicodemus alisema shirika hilo linahamasisha matumizi ya mbinu za kilimo zinazolinda mazingira, ikiwemo matumizi ya mbolea za asili, utunzaji wa mbegu bora na matumizi ya teknolojia zinazoongeza uzalishaji bila kuathiri mazingira.
Mbali na sekta ya kilimo, alisema IFTz inatoa mafunzo ya ufugaji wa kisasa, hususan ufugaji wa mifugo na nyuki, ili kuwasaidia wananchi kupata vyanzo mbadala vya kipato kupitia uzalishaji wa asali na bidhaa nyingine zitokanazo na mifugo.
Aidha, alisema shirika hilo linawahamasisha wakulima kuongeza thamani ya mazao yao kwa kuyachakata na kutengeneza bidhaa zenye ushindani sokoni, hatua ambayo husaidia kuongeza mapato na kuibua fursa za ajira.
Alibainisha kuwa IFTz pia inatoa elimu kuhusu uhifadhi wa mbegu za asili, matumizi sahihi ya rasilimali za mazingira pamoja na ustawi wa mifugo kupitia maarifa kuhusu lishe, afya, malisho na makazi bora ya wanyama.
“Mafanikio ya sekta ya kilimo na mifugo yanategemea uwepo wa sera na kanuni rafiki, ndiyo maana linaendelea kushirikiana na Wizara ya Mifugo na wadau wengine kutoa mapendekezo yatakayoboresha ustawi wa mifugo na maendeleo ya wafugaji nchini,” alisema.
Shirika hilo limewaalika wananchi kutembelea banda lake katika Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu, kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo na ufugaji, pamoja na kufahamu fursa za kiuchumi zinazoweza kuwainua kupitia shughuli za uzalishaji.

More Stories
Mbolea ya fomi yaleta neema kwa wakulima
Msichana Initiative yawajengea uwezo Waandishi wa habari kupinga ndoa za Utotoni
Takwimu sahihi zatajwa nguzo muhimu maendeleo ya Taifa