Na Joyce Kasiki, Dodoma
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimebuni mfumo unaotumia teknolojia ya blockchain kuongeza uwazi, uaminifu na ufanisi katika mnyororo wa ugavi wa mazao ya kilimo, hususan katika mfumo wa usimamizi wa stakabadhi za maghala na kilimo cha mkataba.
Akizungumza katika Maonesho ya Wakulima Nanenane katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma, Mtafiti Mkuu wa mradi huo kutoka UDOM, Dkt. Hilda Mwangakala, alisema ubunifu huo umetokana na matokeo ya tafiti zilizobaini changamoto zinazowakabili wakulima katika mifumo hiyo miwili.
Alisema katika mfumo wa usimamizi wa stakabadhi za maghala, utafiti ulibaini changamoto za ukosefu wa uwazi katika bei za minada, kiwango kidogo cha uaminifu kati ya wadau pamoja na makato ambayo wakulima wengi hawapati maelezo ya kutosha.
Kwa upande wa kilimo cha mkataba, Dkt. Mwangakala alisema changamoto kubwa ni ukosefu wa uwazi katika upangaji wa bei pamoja na kutokuwepo kwa usawa wa nguvu za maamuzi kati ya wakulima na wanunuzi.
Alisema mfumo huo wa blockchain unahifadhi taarifa katika vituo mbalimbali (nodes) kwa wakati mmoja na kuzisambaza kwa wadau, hatua inayosaidia kuhakikisha taarifa zinakuwa salama, za kuaminika na zisibadilishwe bila idhini.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwangakala, kupitia mfumo huo mkulima ataweza kufuatilia mazao yake kuanzia yanapokusanywa na chama cha msingi, yanapopelekwa kwenye ghala kuu hadi yanapouzwa katika mnada.
Alisema taarifa hizo zitapatikana kupitia simu ya mkononi, huku mkulima akiwa na uwezo wa kufahamu minada ambayo mazao yake yameshiriki, bei iliyopatikana na kiasi cha mazao kilichouzwa.
“Hatua hii itaongeza uwazi na kujenga uaminifu kati ya wakulima na wadau wengine wa sekta ya kilimo,” alisema.
Dkt. Mwangakala aliongeza kuwa mfumo huo umeboreshwa kwa kutumia mikataba janja (smart contracts) katika kilimo cha mkataba, ambapo masharti yaliyokubaliwa yatatekelezwa kiotomatiki baada ya kila upande kutimiza wajibu wake.
Alisema mkulima akitimiza vigezo vilivyowekwa kwenye mkataba, malipo yatafanyika moja kwa moja kupitia benki, huku mnunuzi naye akitekelezewa masharti yake kwa mujibu wa mkataba.
Kwa mujibu wa mtafiti huyo, mfumo huo unatarajiwa kupunguza migogoro, kuongeza uwazi na kuimarisha ufanisi katika biashara ya mazao ya kilimo.

More Stories
Kituo cha Saratani kuwa kimbilio kwa wananchi Mbeya
Waziri Kabudi:Serikali itaendelea kuthamini mchango wa Lukuvi
Mkenda:Ujuzi agenda kuchochea ajira kwa vijana