August 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UWT yahimiza matumizi ya mikopo ya asilimia kumi



MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Mary Pius Chatanda (MCC), amevipongeza vikundi vya wanawake katika Halmashauri ya Kyela kwa umahiri, ubunifu na kasi yao ya ujasiriamali kupitia matumizi sahihi ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali kupitia halmashauri.

Amevitaja vikundi vya Tubhagile Kikusya na Juhudi Vikoba Itunge kuwa mfano wa kuigwa kutokana na uaminifu wao katika kukopa, kurejesha mikopo kwa wakati na kuendelea kukopa kwa lengo la kukuza mitaji ya biashara zao.


Amesema mafanikio yaliyopatikana kupitia vikundi hivyo yamewawezesha wanawake kujitegemea kiuchumi kwa kuendesha biashara mbalimbali zikiwemo za mchele, saluni, maduka ya rejareja na magenge ya vyakula, hatua inayochangia kuongeza kipato cha familia na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa. Chatanda ameyasema hayo leo, Agosti 5, 2026, wilayani Kyela, mkoani Mbeya.


Katika hotuba yake, Chatanda ametoa wito kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambao bado hawajajiunga na vikundi vya kiuchumi au kunufaika na mikopo ya asilimia 10 kujitokeza na kutumia fursa hiyo ili kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.


Aidha, amewahimiza wanawake kuendelea kuhamasishana katika maeneo mbalimbali ya kijamii, ikiwemo mikutano, saluni na nyumba za ibada, ili kuongeza uelewa kuhusu fursa za uwezeshaji wa kiuchumi zinazotolewa kupitia mikopo ya asilimia 10.


“Wanawake tusaidiane kuhamasishana katika mikutano, saluni na makanisani ili kila mwanamke apate uelewa na kunufaika na fursa hizi za uwezeshaji kupitia mikopo ya asilimia 10,” amesema Chatanda.


Pia ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kusimamia na kuimarisha programu zinazowawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi.


Chatanda ameanza jana ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya, akiwa ameambatana na ujumbe wake kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 katika Halmashauri ya Kyela, pamoja na kufanya mikutano ya ndani na wanachama wa CCM.