Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbeya
Kutoka katika ugumu,visa mikasa na ndoto ya mbunifu, Adam Zacharia hatimaye ameona mwanga baada ya Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH),kutoa zaidi ya sh.milioni 96.
Hatua hiyo imemvusha kutimiza ndoto yake ya ubunifu wa kutengeneza mashine za kisasa za kuchakata mazao mahindi na kuchonga vipuri vya magari aina mbalimbali.
Zacharia anasema,katika safari yake ya kutimiza ndoto yake ilikuwa na milima na mabonde ambayo COSTECH imemwinua na kufikia malengo yake ya kuisaidia jamii katika kuondokana na changamoto katika sekta ya kilimo.
“Ndoto yangu na matamanio ni kuisaidia jamii katika sekta ya kilimo,lakini awali nilianza na mashine inayo tembea(mobile garage),nikiwa na lengo na kujitafutia kipato cha kujikwamua kiuchumi,”anasema Zacharia.

Anasema ugumu wa maisha kwake ulifikia kikomo mwaka 2019,baada ya COSTECH kumtambua kwenye maonesho ya bunifu yaliyo shirikisha makundi mbalimbali kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini.
Pia anasema baada ya mashindano walikutanishwa ambapo kila mmoja alieleza mahitaji yake,ambapo yeye alieleza changamoto ni kupata vifaa na mashine za kisasa.
Hivyo upatikanaji wa vifaa hivyo ulifungua milango ya safari mpya ya kuboresha ubunifu kwa kutengeneza mashine za kuchakata mazao mchanganyiko zenye ubora tofauti na za nje nchi.
Gharama za kuchakata.
Zacharia anasema,wastani kwa siku inachakata gunia 1,000 sawa na tani moja jambo ambalo limewapungizia muda wakulima walio wengi .
“Teknolojia hiyo imekuwa mkombozi kwa wakulima kwani inapunguza muda pamoja na kuajiri vibarua kuchakata na kuhifadhi kwenye maeneo rasmi,”anasema.
Hata hivyo, Zacharia anasema mbali na kuchakata mazao pia kupitia uwekezaji huo wa COSTECH umesaidia kuwezesha ongezeko la ajira kwa vijana na kupokea wengine kutoka kwenye vyuo mbalimbali kujifunza kwa vitendo.
“Nimepokea vijana wengi kutoka vyuo mbalimbali vya Serikali,ambapo wengine kwa sasa wamefika mbali kiuchumi na kuwa na miradi yao ambayo imekuwa ikiwaongozea kipato,”anasema.
Mbali na mafanikio hayo anasema kuwa kuna changamoto mbalimbali za usajili wa bidhaa jambo ambalo linakwamisha katika masoko ya nje.
Ombi
Katika hatua nyingine ameiomba COSTECH kuwaongezea ujuzi ili kuwawezesha kwenda mbali zaidi katika kufanya ubunifu wenye matokeo makubwa katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Zacharia anasema Serikali inapo waunga mkono wabunifu na wakapata faida wanahamasika kulipa kodi.
Anasema,baada ya kuwezeshwa mashine amekuwa mlipa kodi mzuri wa hapa nchini,huku akiishukuru COSTECH na Serikali kwa kumfikisha hapo alipo.
Kauli ya COSTECH
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha kuendeleza na kuhaulisha teknolojia kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi Tanzania (COSTECH)Dkt.Erasto Mlyuka anasema, Serikali ilivutiwa na teknolojia ya mbunifu huyo,hivyo ikampatia vifaa vyenye thamani ya sh.milioni. 60 ili kuendeleza vijana wengine.
“Kupitia mfuko wa Rais Samia wa ubiasharishaji ubunifu Suluhu Hassan, kuna zaidi ya sh.bilion .4 kwa ajili ya kuendeleza bunifu za vijana ili kuleta tija katika sekta ya kilimo,”anasema Dkt.Mlyuka.
Hata hivyo Dkt.Mlyuka anasema, jukumu lao ni kuona namna bora ya kuwawezesha wabunifu kufikia ndoto za kuhuhuisha teknolojia zinazokwenda sambamba na uhitaji wa masoko.
Anasema kuwa pamoja na kuwaunganisha na taasisi za kisayansi na teknolojia katika kuelekea miaka 40 ya COSTECH,watahakikisha wabunifu na watafiti wanafikiwa na fursa mbalimbali ili kuleta mapinduzi katika nyanja za sekta ya kilimo na nishati.
Aidha anasema, kitu cha kujivunia kwa miaka 40, COSTECH huo ni umri wa mtu mzima na kueleza kuwa kuna mashine ya mil.60.ipo kwa mbunifu mmoja lakini imeleta manufaa kwa vijana wengi wa maeneo ya jirani.
“Hivyo Serikali ndivyo inavyojipambanua kusema wanawasaidia watu wake kutokana na mtu mmoja kujitoa kusaidia watu wengine.Na haya mazingira mnayoona siyo kwamba yapo tu Songwe yapo karibu kila mkoa ambapo wamekuwa na vituo vya kiteknolojia ,kumbi bunifu,”anasema.
Dkt.Mlyuka anasema kwamba,kuna maeneo ambayo wamekuwa wakijivunia kwa kukaa kwenye mnyororo.

Kwa upande mmoja wa mnufaika wa mbunifu huyo ,Enerst Makanga,ameishukuru tume hiyo kwa uwekezaji wa mashine hizo na kusaidia kundi la vijana kupata fursa ya kujifunza.
Makanga anasema,kupitia kazi hiyo imekuwa msaada kwake katika kujinua kimaisha hivyo anaiheshimu kwani imeweza kumtoa mbali mpaka kufika hapo.
“Mimi hapa ni fundi lakini kupitia hii kazi, wamekuwa wakirahisisha watu kwenda nje ya nchi lakini kupitia wao kazi imekuwa ikienda kwa wakati na kwa muda mfupi,”anasema Makanga.
Mwisho.

More Stories
IFTz yaongeza tija kwa wakulima kupitia Teknolojia rafiki
UWT yahimiza matumizi ya mikopo ya asilimia kumi
TMDA yahamasisha viwanda vya dawa za mifugo