August 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yahakikisha vyakula vya samaki havileti madhara

Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

IMEELEZWA kuwa Serikali imechukua na itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha vyakula vinavyotumika kulisha samaki wanaofungwa havihatarishi afya ya walaji wala kuharibiwa mazingira ya Ziwa Victoria.

Huku ikisisitiza matumizi sahihi ya vyakula vya samaki,uzingatiaji wa kiwango stahiki cha kulisha samaki na msongamano unaokubalika wa samaki wa vizimba,hatua inayopunguza mabaki ya chakula na virutubisho vinavyoweza kuchafua maji na hivyo kuhifadhi ubora wa mazingira wa Ziwa Victoria.

Hayo yameelezwa na Agosti 5,2026 na Mkuu wa Idara ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi Simon Langoi, akijibu swali kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Ummy Wayayu, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo katika kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmshauri hiyo cha kujadili robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Ambapo swali hilo liliulizwa na Diwani wa Viti Maalumu Rahma Hital,aliyetaka kufahamu ,je Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha kuwa vyakula vinavyotumika kulisha samaki wanaofungwa ziwani haviathiri afya ya walaji na wakati huo huo haviathiri mazingira ya Ziwa Victoria.

Langoi amesema,vyakula vinavyozalishwa au kuingizwa nchini hukaguliwa na mamlaka zenye dhamana ikiwemo Mamlaka ya Viwango Tanzania(TBS) na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Idara ya Uvuvi.

“Pale inapohitajika uchunguzi wa kimaabara,ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali hufanya uchambuzi wa sampuli ili kubaini kama chakula hicho kinakidhi viwango vya usalama na hakuna kemikali au viambatano vinavyoweza kuhatarisha afya ya walaji na mazingira,”amesema Langoi.

Pia amesema, Serikali kupitia mamlaka husika hufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa wazalishaji,wasambazaji na wafugaji wa samaki ili kuhakikisha vyakula vinavyotumika vinazingatia viwango vilivyowekwa na havina viambato vinavyoweza kuhatarisha afya ya binadamu au mazingira.

Hata hivyo amesema,Serikali huchukua hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria ya uvuvi,kanuniza ufugaji wa samaki,sheria ya viwango na sheria nyingine husika pale inapobainika kuna uzalishaji au usambazaji wa vyakula vya samaki visivyokidhi viwango.

Sanjari na hayo amesema, wataalamu wa uvuvi wanaendelea kutoa elimu na ushauri wa kitaaluma kwa wafugaji kuhusu matumizi ya vyakula vilivyoidhinishwa,mbinu bora za ufugaji na usimamizi wa vizimba ili kulinda afya ya samaki,usalama wa walaji na mazingira ya Ziwa Victoria.

“Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kuna vizimba 267, vinavyotumika kufugia samaki ziwani na mabwawa 47, ili kuhakikisha shughuli hizi zinaendelea kwa tija na usalama,matumizi ya chakula bora na salama cha samaki ni miongoni mwa masharti muhimu yanayosisitizwa na Serikali,”.