Na Jotxe Kasiki,Dodoma
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeendelea kuonesha mchango wake katika kukuza sekta ya ufugaji nyuki kwa kubuni bidhaa mbalimbali zinazotokana na mazao ya nyuki, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao hayo, kutatua changamoto za jamii na kufungua fursa za ajira na biashara.
Akizungumza katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma, mwanafunzi wa Ndaki ya Sayansi za Kilimo na Teknolojia ya UDSM, Josiana Donald, alisema chuo hicho kinafanya ufugaji wa nyuki wakubwa na nyuki wadogo sambamba na kufanya tafiti zinazowezesha mazao ya nyuki kutumika kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye manufaa kwa jamii.
Alisema mbali na kuzalisha asali ya nyuki wakubwa na nyuki wadogo, UDSM pia imefanikiwa kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo dawa ya kikohozi, dawa ya kung’arisha viatu (Royal Spray Shoe Polish), shower gel na sabuni za mikono zinazotokana na mazao ya nyuki.
Kwa mujibu wa Donald, dawa ya kikohozi imetengenezwa kwa kutumia asali ya nyuki wadogo iliyochanganywa na tangawizi pamoja na viambato vingine vya tiba asili, jambo linalosaidia kupunguza kikohozi, mafua na changamoto nyingine za mfumo wa upumuaji.
Aidha, alisema dawa ya kung’arisha viatu imetengenezwa kwa kutumia nta ya nyuki wakubwa na hutoa mwonekano mzuri pamoja na kuongeza ubora wa viatu.
Aliongeza kuwa shower gel na sabuni za mikono zinazozalishwa kwa kutumia asali husaidia kulinda ngozi, kuongeza unyevunyevu na kupunguza matumizi ya kemikali zinazoweza kuathiri afya ya ngozi.
Donald alisema ubunifu huo umetokana na kutambua kuwa wafugaji wengi huuza mazao ya nyuki bila kuyaongezea thamani, hali inayowanyima fursa ya kuongeza kipato na kupanua masoko ya bidhaa zao.
Alibainisha kuwa kupitia tafiti na ubunifu huo, UDSM imeonesha kuwa mazao ya nyuki yanaweza kutumika kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye soko na mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.
Aliwataka wawekezaji, taasisi za elimu, watafiti na wananchi kutembelea banda la UDSM katika Maonesho ya Nane Nane ili kujifunza kuhusu teknolojia za ufugaji nyuki, bidhaa zinazotokana na mazao ya nyuki na fursa zilizopo katika sekta hiyo.

More Stories
Chatanda ahamasisha utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025–2030
Mikopo asilimia 10 yainua wanawake Tunduma kibiashara
Airtel  yaimarisha ushirikiano  wa Airtel Business Monthly Mug TournamentÂ