Na Mwandishi wetu
TUME ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imesema inatarajia kuanza zoezi kubwa la ugawaji wa pampu za maji katika mikoa saba nchini, ambapo uzinduzi rasmi wa mpango huo unatarajiwa kufanyika mkoani Katavi Agosti 11 mwaka huu.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa wakati akizugumza na waandishi wa wa habari katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea Jijini Dodoma.
Amesema jumla ya pampu za kawaida 1,000 zitatolewa kwa wakulima wa mbogamboga na matunda ili kuwawezesha kuvuta maji kwa urahisi kutoka kwenye mito na mabonde kwa njia salama isiyoharibu mazingira.
“Tume imenunua zaidi ya pampu 1,000 za kisasa zinazotumia nishati ya jua (solar pumps) ambazo zitatolewa kwa wakulima wa zao la parachichi ili kuongeza ufanisi wa uzalishaji”amesema
Vilevile amesema Tume hiyo pia imeandaa mradi mkubwa wa uchimbaji wa visima utakaotoa ajira kwa vijana kati ya 2,000 na 4,000 ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Ameongeza kuwa mpango huo utahusisha uundaji wa vikundi vya vijana wenye ujuzi wa ufundi na uhandisi katika halmashauri zote 184 nchini.
Aidha amesema hadi sasa Tume tayari imechimba visima 415, huku ikilenga kufikia visima 67,000 ndani ya kipindi cha miaka minane ijayo.
Katika hatua nyingine amesema Tume hiyo imefanikiwa kusimamia mikataba 146 ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, ambapo wakandarasi wanaendelea na utekelezaji wa kazi katika maeneo mbalimbali nchini.

More Stories
VETA yaleta suluhisho uharibifu wa Parachichi
Mahundi awataka vijana kukemea uchochezi na kuitetea serikali
VETA Singida yahamasisha utengenezaji bora wa Silaji Tanzania