Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya
MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere, amewataka maafisa ugani nchini kuendelea kutoa elimu kwa wakulima ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuwawezesha kunufaika na masoko ya kimataifa.
Makongoro ametoa kauli hiyo leo Agosti 3, 2026, alipotembelea banda la Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea kikanda kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Akiwa kwenye banda hilo, alijionea bidhaa mbalimbali za kilimo zilizoletwa na wakulima pamoja na mbinu za kilimo cha kisasa zinazotekelezwa na halmashauri hiyo.
Amesema Tanzania ina uwezo wa kujitosheleza kwa chakula, lakini bado kuna umuhimu wa maafisa ugani kuendelea kuwapa wakulima elimu ya mbinu bora za uzalishaji ili kuongeza ubunifu, tija na ushindani wa mazao katika masoko ya nje.

“Tanzania ina ziada ya chakula,Sasa jukumu letu ni kuongeza uzalishaji wenye tija ili kunufaika na masoko ya nje na kuongeza kipato cha wakulima pamoja na mapato ya serikali,” amesema.
Makongoro ametolea mfano wa miaka mitatu iliyopita wakati Zambia ilipokumbwa na ukame, ambapo Serikali ya Tanzania iliruhusu uuzaji wa mazao nchini humo na hivyo kutoa fursa kwa wakulima wa mikoa ya Rukwa na Katavi kuuza mazao yao na kupata soko la uhakika.
Amesisitiza kuwa wakulima wanapaswa kuongeza uzalishaji wa mazao na mifugo pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa zao ili kukidhi mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa maandalizi mazuri ya banda lake katika maonesho hayo.
“Niwapongeze sana Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa jinsi mlivyojipanga katika maonesho haya. Hata mazao na vipando mlivyoonesha vina ubora mkubwa mnastahili pongezi,” amesema .

Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Cuthbert Mwinuka, amesema halmashauri imetenga zaidi ya Sh milioni 30 kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu bora za shayiri ambazo tayari zimepata soko kupitia Kiwanda cha Serengeti.
Amesema mbegu hizo zitatolewa kwa wakulima kwa utaratibu wa ruzuku ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kimkakati, ikiwemo shayiri, pareto na kahawa, sambamba na kuendelea kutoa elimu ya kilimo bora kwa wananchi.

More Stories
NIRC yatangaza neema kwa Wakulima Nanenane
DCEA yateketeza hekari 3,117.9 mashamba ya bangi Lindi
Ufadhili wa TADB waimarisha Viwanda vya Kilimo