August 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tozo ya mafuta yaboresha barabara Mwanza

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

IMEELEZWA kuwa fedha zinazotokana na tozo ya sh.100 kwa kila lita ya mafuta ya dizeli na petroli pamoja na Mfuko wa Barabara zimeendelea kuimarisha ujenzi na matengenezo ya barabara Mkoa wa Mwanza, huku zikichangia kufunguliwa kwa mtandao mpya wa barabara na kuboresha huduma za usafiri.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Mwanza Mhandisi Makori  Kisare,wakati akizungumza  na Majira ofisini kwake jijini hapa,ambapo amesema taasisi hiyo ina vyanzo vitatu vikuu vya fedha vinavyowezesha utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara.

Amesema chanzo cha kwanza ni Mfuko wa Barabara ambao hutumika zaidi kugharamia matengenezo ya kawaida na maeneo korofi ili kuhakikisha barabara zilizopo zinaendelea kuwa katika hali nzuri au bora zaidi.

Ameeleza kuwa chanzo cha pili ni tozo ya sh.100 kwa kila lita ya mafuta ya dizeli na petroli,ambayo hutoa fursa ya kugharamia ujenzi wa barabara mpya pamoja na matengenezo ya zilizopo kulingana na mahitaji.

Aidha,amesema Serikali kupitia Mfuko Mkuu hutenga kiasi cha sh milioni.500 kwa kila jimbo kila mwaka kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara, fedha ambazo si za Mfuko wa Jimbo bali ni bajeti ya Serikali.

Kwa mujibu wa Mhandisi  Kisare,TARURA Mkoa wa Mwanza hupokea wastani wa bajeti ya kati ya sh.bilioni 23 na sh.bilioni 25 kila mwaka, ikiwemo sh.bilioni 8.9 kutoka Mfuko wa Barabara,sh.bilioni 9.1 kutoka tozo ya mafuta na sh.bilioni 4.5 za fedha za majimbo tisa ya Mkoa huo,ambapo kila Jimbo hupatiwa sh milioni 500 huku mwaka 2025/2026 ilipokea sh.bilioni 1.9 kutoka mapato ya ndani ya Halmshauri ya Jiji la Mwanza.

Amesema mtandao wa barabara unaosimamiwa na TARURA mkoani humo una urefu wa kilomita 8,586 zenye viwango tofauti vya ujenzi.

Amefafanua kuwa kati ya hizo, kilomita 99.8 ni za lami, kilomita 11.4 ni za zege kutokana na jiografia ya Mkoa wa Mwanza, kilomita 18.7 zimejengwa kwa mawe, kilomita 1,797 ni za changarawe na kilomita 6,659 ni za udongo.

Aidha amesema kutokana na upatikanaji wa fedha hizo, TARURA imeendelea kufungua barabara mpya na kuboresha zilizopo, huku ikipanga vipaumbele vya utekelezaji kwa kushirikiana na Mabaraza ya Madiwani na wadau wengine wa maendeleo.