July 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Elimu usalama barabarani yatolewa kwa askari wa JWTZ

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza 

JESHI la Polisi  Mkoa wa Mwanza kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani,limetoa elimu ya usalama barabarani pamoja na huduma ya ukaguzi wa hiari wa magari kwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha MTC.

Akizungumza Julai 22,2026 mara  baada ya utolewaji wa elimu hiyo, MP Kamanda wa Mwanza Transit Camp,Kapteni Frank Machera,amesema elimu hiyo inaendana na agizo la Serikali linalomtaka kila mmiliki na dereva wa chombo cha moto kukamilisha taratibu za Wiki ya Nenda kwa Usalama hadi kupata stika ya uthibitisho.

Pia amesema,elimu hiyo  iliyotolewa kwa askari wa JWTZ Kikosi cha MCT pamoja na huduma ya ukaguzi wa magari kupitia mfumo wa MIMIS,itasaidia kupunguza ajali na migongano inayoweza kutokea barabarani.

Kapteni, Machera amesema,uwepo wa wataalamu wa usalama barabarani katika eneo la kikosi hicho kwa ajili ya kutoa huduma ya ukaguzi umewasaidia kuokoa muda wa kwenda vituo vya polisi kufuata huduma hiyo.

Akitoa elimu kuhusu mfumo wa ukaguzi wa magari wa MIMIS, S/SGT Christopher Miku kutoka Dawati la Elimu Ofisi ya Mkuu wa Usalama Barabarani (RTO) Mwanza amesema, mfumo huo umeboreshwa ambapo maombi na uthibitisho wa ukaguzi vinafanyika kwa njia ya mtandao badala ya kutumia stika za karatasi.

Amesema endapo gari litabainika kuwa na hitilafu, mmiliki atatakiwa kufanya marekebisho na kulirejesha kwa ukaguzi bila kulipa tena ada ya awali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, SSP Sunday Ibrahim, amewataka askari, wamiliki na madereva wa vyombo vya moto kutumia huduma ya ukaguzi wa hiari angalau mara moja kwa mwaka katika kipindi cha Wiki ya Nenda kwa Usalama.

Amesema hatua hiyo inalenga kujenga utamaduni wa kutii sheria bila shuruti, kupunguza migogoro kati ya madereva na askari pamoja na kuimarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara.

Kauli mbiu ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani mwaka huu  inasema “Familia yako inakusubiri, zingatia sheria”.