July 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania,Misri zaainisha maeneo ya Kipaumbele ya Ushirikiano wa Maendeleo


Na Penina Malundo,Timesmajira


Tanzania na Misri zimeainisha maeneo ya kipaumbele ya ushirikiano yatakayolenga
kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika bandari, usafirishaji, kilimo, nishati,
maji na viwanda ili kukuza biashara, uwekezaji na ajira katika nchi hizo mbili.


Hayo yamebainishwa jana Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara ya kitaifa ya Rais wa
Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mheshimiwa Abdel Fattah El-Sisi nchini kwa mwaliko wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Rais Dkt. Samia amesema uhusiano wa kihistoria wa Tanzania na Misri unapaswa sasa
kutafsiriwa katika miradi inayoonekana na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wa
pande zote mbili, akibainisha kuwa kiwango kilichopo cha biashara hakiakisi ukubwa wa
uchumi na fursa zilizopo katika nchi hizo.


Katika uchukuzi, Tanzania imeikaribisha Misri kuwekeza katika uendelezaji wa Bandari ya
Dar es Salaam na ujenzi wa miundombinu ya Bandari ya Bagamoyo, ikiwemo njia ya reli
itakayoiunganisha na Kongani ya Viwanda ya Kwala na Reli ya Kisasa (SGR).


Pande hizo mbili zimeeleza dhamira ya kuimarisha ushirikiano katika kuunganisha bandari
zao, kuanzisha huduma za usafiri wa baharini na kujenga vituo vya kisasa vya kuhifadhi
na kusambaza mizigo.


Ushirikiano huo unatarajiwa kuunganisha masoko ya Afrika Mashariki na Kusini na Misri,
Mashariki ya Kati, Asia na Ulaya kupitia Bahari ya Hindi, Bahari ya Shamu, Mfereji wa Suez
na Bahari ya Mediterania.


Kadhalika, Tanzania imeainisha kilimo, mifugo na uvuvi kuwa miongoni mwa maeneo
yenye fursa za kupanua ushirikiano na Misri katika umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu,
uvunaji wa maji ya mvua, ufugaji wa kisasa na viwanda vya kuchakata mazao.



Vilevile, imeikaribisha Misri kuwekeza katika eneo la Ranchi ya Ruvu na kushirikiana na
Jeshi la Kujenga Taifa, Magereza na Shirika la Chakula la Taifa katika miradi ya uzalishaji
wa chakula, mifugo na bidhaa zitokanazo na mifugo.


Rais El-Sisi amesema Misri ipo tayari kushiriki katika mradi mkubwa wa kilimo
utakaoendeshwa kwa ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi ili kuimarisha usalama wa
chakula na kuongeza biashara ya mazao.


Katika elimu, Misri imeeleza utayari wa kutoa nafasi za ufadhili kupitia Mpango wa
ufadhili wa masomo wa Samia Scholarship katika fani za sayansi, tiba, akiliunde, TEHAMA
na usalama wa mtandao.


Aidha, katika afya, nchi hiyo pia imeonesha utayari wa kujenga au kukarabati hospitali
itakayopendekezwa na Serikali ya Tanzania na kutoa mafunzo katika upasuaji wa moyo,
figo, ini, saratani na huduma nyingine za kibingwa.


Marais hao pia wameshuhudia utiaji saini wa hati mbili za makubaliano kuhusu
ushirikiano katika umeme na nishati jadidifu, pamoja na sekta mbalimbali za uchukuzi.
Rais Dkt. Samia amesema mafanikio ya mazungumzo hayo yatapimwa kwa kasi ya
utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano yaliyobainishwa.


“Tumekubaliana kwenda kwa haraka. Tunachohitaji sasa ni kuaminiana, kufanya
maamuzi na kutekeleza tuliyokubaliana bila kuchelewa,” amesema.


Katika hatua nyingine, viongozi hao wamefunga Jukwaa la Biashara na Uwekezaji la
Tanzania na Misri lililowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi zote
mbili.


Rais Dkt. Samia amezialika kampuni zaidi za Misri kuwekeza Tanzania, akisema mazingira
ya biashara ni rafiki na fursa zilizopo ni nyingi.
“Mustakabali wa Afrika utajengwa na biashara za Afrika zinazowekeza Afrika,”
amesema Rais Dkt. Samia.


Kwa upande wake, Rais El-Sisi amesema ushirikiano wa kiuchumi utaelekezwa katika
bandari, usafiri wa baharini, reli, maeneo ya viwanda, miundombinu, teknolojia na kilimo,
huku sekta binafsi ikiongoza uwekezaji wenye thamani ya nyongeza.


“Tunategemea sekta binafsi kujenga miradi itakayofungua fursa mpya za maendeleo na
ustawi kwa wananchi wa nchi zetu mbili,” amesema Rais El-Sisi.


Misri inashika nafasi ya nane miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uwekezaji nchini
Tanzania, ikiwa na miradi 61 yenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 1.5,
iliyozalisha zaidi ya ajira 4,000 katika nishati, viwanda, ujenzi, kilimo, utalii na huduma.