Na Joyce Kasiki, Dar es Salaam
TUME ya Ushindani Tanzania (FCC) imewahimiza wananchi kutumia fursa ya Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kupata elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo, ikiwemo usajili wa mikataba, kupokea na kusikiliza malalamiko pamoja na elimu kuhusu bidhaa bandia.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa FCC, Roberta Feruzi, alisema taasisi hiyo inatoa huduma papo kwa hapo kwa wateja wanaotembelea banda lao, huku ikiendelea kutoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara kuhusu masuala ya ushindani wa biashara na ulinzi wa mlaji.
Alisema FCC imetumia maonesho hayo kama jukwaa la kuwafikia makundi mbalimbali ya wafanyabiashara, wajasiriamali na wadau wengine wa sekta ya biashara kwa lengo la kuwaongezea uelewa kuhusu sheria, huduma na majukumu ya taasisi hiyo.
“Tunatoa semina mbalimbali kila siku kwa wafanyabiashara wanaoshiriki maonesho haya ili kuwajengea uwezo na kuwapa elimu kuhusu ushindani wa haki sokoni pamoja na namna ya kutambua na kupambana na bidhaa bandia,” alisema Feruzi.
Aliongeza kuwa utoaji wa elimu hauishii katika banda la FCC pekee, bali taasisi hiyo imekuwa ikiwafuata wadau walipo ndani ya maonesho hayo na itaendelea na kampeni za utoaji elimu hata baada ya maonesho kumalizika.
Feruzi alisema juhudi hizo zinaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi jumuishi kwa kuhakikisha wafanyabiashara na wajasiriamali wanapata mazingira bora ya kufanya biashara na kushindana kwa haki.
Aliwataka wananchi na wadau wote kutembelea banda la Wizara ya Viwanda na Biashara, ambalo linawakutanisha taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo, ili kupata huduma na elimu mbalimbali zinazotolewa na FCC pamoja na taasisi nyingine.

More Stories
DC awataka viongozi wa serikali za wanafunzi kulinda amani
Usalama waimarisha Mwanza
Hati miliki 527 zakabidhiwa kwa wananchi