July 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC awataka viongozi wa serikali za wanafunzi kulinda amani

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline,
Mbeya

MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amewataka viongozi wa serikali za wanafunzi wa Vyuo na Vyuo vikuu pamoja na viongozi wa matawi kuwa mfano wa kuhamasisha na kulinda amani na utulivu katika taasisi zao.

Amesema viongozi hao wana wajibu wa kuendeleza imani waliyopewa na wanafunzi waliowachagua kwa kuwatumikia kwa uadilifu, uzalendo na kuwahamasisha kudumisha amani wakati wote.

Itunda ametoa wito huo Julai 6, 2026 alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu pamoja na viongozi wa matawi kutoka mkoani humo.

“Nawasisitiza ndugu zangu, nendeni mkawa mabalozi wa kulinda amani na utulivu katika maeneo yenu ya vyuo na vyuo vikuu. Wanafunzi waliowachagua wana imani kubwa kwenu, hivyo tumieni nafasi zenu kuhimiza mshikamano na uwajibikaji,” amesema Itunda.

Aidha, amewataka viongozi hao na wanafunzi kwa ujumla kuendelea kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi, kielimu na kijamii zinazopatikana ndani ya Mkoa wa Mbeya ili kujiongezea maarifa na kujiletea maendeleo hata wanapokuwa chuoni.

Alisisitiza kuwa matumizi sahihi ya fursa hizo yatawasaidia vijana kujijengea uwezo na kuchangia maendeleo ya taifa sambamba na kudumisha amani na utulivu.

Raphael kandonga mkazi wa Sai amesema kuwa amani iliyopo inapaswa kulindwa hivyo kila mwananchi ana awajibu wa kulinda amani na utulivu uliopo.