July 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ummy ahimiza wenye ulemavu kujumuishwa

Na Joyce Kasiki, Dar

NAIBU Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Watu Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga, ametoa wito kwa taasisi za umma na binafsi kuendelea kuzingatia ujumuishi wa watu wenye ulemavu katika utoaji wa huduma, ajira na fursa za kiuchumi ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika maendeleo ya Taifa.

Ameyasema hayo alipotembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Sabasaba, jijini Dar es Salaam.

Ummy alipata fursa ya kujionea huduma na programu mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Ummy amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki na fursa sawa katika nyanja zote za maendeleo, huku akizitaka taasisi na kampuni binafsi kushirikiana na Serikali katika kutekeleza sera na sheria zinazolenga kukuza usawa na ujumuishi.

“Naendelea kuwashukuru wote kwa pongezi mnazoipa Serikali kwa kazi inayoendelea kufanyika. Hata hivyo, ni muhimu zaidi kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na uchumi.

Tunaziomba taasisi na kampuni zote kushirikiana nasi ili kujenga mazingira jumuishi yatakayowawezesha wananchi wote kunufaika na fursa zilizopo,” amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vinavyowakabili watu wenye ulemavu katika kupata huduma mbalimbali, akieleza kuwa ujumuishi si suala la kundi fulani pekee bali ni wajibu wa jamii nzima.