July 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Homera ashitushwa kina Mama kutozwa fedha baada ya kujifungua

Na Israel Mwaisaka, Rukwa

‎Waziri wa Sheria na Katiba Dkt,Juma Homera amesikitishwa na kitendo kinachofanywa na Watumishi wa hospitali ya wilaya Sumbawanga ya kuwatoza Mama wanaojifungua Watoto katika hospitali hiyo ambapo Mama anayejifungua mtoto wa kiume utozwa Tshs,10,000 na kwa mtoto wa kike utozwa Tshs,5,000

‎Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Jana katika kata ya Mtowisa alisema kuwa taarifa hizo zimemsikitisha na kuitaka taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa kuchukua hatua za haraka juu ya tuhuma hizo kwa maana hilo halikubaliki.

‎Alisema kuwa sera ya afya inajieleza vizuri juu ya huduma kwa Mama wajawazito na Watoto chini ya miaka mitano na kuwa katika sera hiyo hakuna mahala panapoeleza kwamba Mama akijifungua mtoto wa kiume au wa kike kutozwa kiasi chochote Cha Fedha na kuwa huo ni uwizi hivyo TAKUKURU wachukue hatua juu ya Watumishi hao wa afya.

‎Awali Wananchi wa kata hiyo ya Mtowisa walimweleza Waziri Homera kwamba wamekuwa wakitozwa tozo mara baada ya Mama kujifungua na kuwa pale inapotokea Mama kujifungua mtoto wa kiume utozwa kiasi kikubwa Cha Fedha Cha Tshs,10,000 na bila ya kupewa risiti yoyote .

‎Walidai kuwa wao wanafahamu kwamba hakuna tozo yoyote pale mama anapokwenda kujifungua Sasa tozo hizo wanazotozwa baada ya kujifungua hawazielewi lakini ulazimika kuzilipa kwa sababu hawana namna yoyote ya kuzikwepa tozo hizo.

‎Pia walieleza kusikitishwa na hospitali hiyo ya wilaya kutokuwepo kwa baadhi ya vipimo muhimu vinavyotakiwa kuwepo katika hospitali ya wilaya na kulazimika kwenda kwenye maabara za Watu binafsi  na kupata vipimo kitu ambacho wameeleza kuwa siyo sahihi.

‎Hivyo Homera aliutaka uongozi wa Wilaya na mkoa kufuatilia changamoto hizo zilizotolewa na Wananchi na kuchukua hatua madhubiti pale watakapobaini uozo huo uliosemwa na Wananchi.

‎Waziri wa  Sheria na Katiba Juma Homera yupo mkoani Rukwa katika ziara ya siku Nne ambapo licha ya shughuli nyingi alizonazo pia anapata fursa ya kuzungumza na Wananchi kupitia mikutano ya hadhara.