July 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri Kyela yavuka lengo la makusanyo,yazuia Lumbesa

Na Israel Mwaisaka,Kyela

‎HALMASHAURI ya wilaya ya Kyela mkoani Mbeya,imefanikiwa kuvuka lengo la makusanyo kwa mwaka 2025–2026 kwa kufikisha asilimia 103 baada ya kukusanya Bilioni 8.8 ukilinganisha na makusanyo ya Bilioni 7.7 ya mwaka uliopita.

‎Akizungumza jana na Waandishi wa habari ofisini kwake ,mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kyela Thobias Mwankonde alisema ushirikiano uliotukuka baina ya madiwani,watendaji na mkurugenzi ndiyo chanzo cha kuvuka lengo.



‎Amesema katika harakati za makusanyo ya mwaka huu ilikuwa ngumu kuvuka lengo kutokana na mtikisiko wa zao la kakao baada ya kukusanya Bil.2.9 ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo wanakusanya Bil. 3.4.

‎Amesema timu ya watendaji wakiongozwa na mkurugenzi mtendaji na ushauri uliotukuka wa mkuu wa wilaya umefanikisha makusanyo hayo na kuwa ili msimu ujao wakusanye zaidi walienda kujifunza wilayani Mbarali namna wanavyokusanya mapato kupitia zao la mpunga.

‎Amesema Kyela wameweka mkakati wa mkulima kutolipa ushuru wa mpunga chini ya tani moja akiwa na kibakli cha utambuzi toka kwa mtendaji wa kata husika kwa wasio na kibali wanalipa ushuru kwenye kizuizi kilichowekwa.

‎Ili kufanya ufanisi katika zao la mpunga,wakiwa mbarali waligundua wenzao walipiga marufuku ujazo wa debe zaidi ya 7 (Lumbesa) ambapo Mbarali kwa mwaka wanakusanya zaidi ya Bilioni 6 kwa mwaka katika zao la mpunga.



‎Aliongeza kuwa ziara hiyo ya wilaya ya Mbarali iliwapa mwanga ambapo wanatarajia kupiga marufuku mifuko yenye ujazo wa bede 10 wakihitaji mifuko ya ujazo wa bede 7 itumike itakayosaidia kukusanya mapato zaidi na kulinda afya za makuli.

‎Aliongeza ujazo wa debe 10 unapunguza nguvu kazi kwa vijana ambao wamekuwa wakiugua na kukohoa damu na wengine kufa pindi wanapobeba mgongoni kwa muda mrefu magunia yenye ujazo wa debe 10.

‎”Ndugu Wanahabari,tumejipanga kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili kukusanya fedha zaidi kuweza kuwahudumia wananchi,ushirikiano kati ya wananchi na viongozi unahitajika kufanikisha hilo”alisema Mwankonde.



‎Danken Mwaisumo mkazi wa Ipinda amesema anaunga mkono jitihada hizo kwani ujazo wa debe 10 ni mkubwa na unawaathiri kiafya vijana wanaobeba mgongoni hivyo ujazo wa debe 7 ukitumika utalinda afya za vijana.

‎Nae Judith Mwampagatwa mkazi wa Bondeni alisema wanafurahi kuona Kyela inang’ara,ofisi mpya ya ghorofa ya mkuu wa wilaya na mkurugenzi inajengwa wilaya inabadirika,na kwamba anaunga mkono jitihada za viongozi za kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuipaisha Kyela.