Na Joyce Kasiki,Dar
NAIBU Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula, amesema takwimu sahihi zina mchango mkubwa katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo, hivyo zimeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema hayo katika banda la Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Luswetula aliipongeza taasisi hiyo kwa kazi nzuri ya kukusanya, kuchambua na kusambaza takwimu zinazosaidia kufanya maamuzi yenye tija.
Alisema ameridhishwa na machapisho na taarifa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo, akieleza kuwa zimekuwa msaada kwa Serikali, watunga sera, wawekezaji na wadau wengine katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Meneja wa NBS Mkoa wa Dar es Salaam, David Danda, alisema taasisi hiyo inafarijika kuona viongozi wa Serikali wanathamini mchango wa takwimu katika maendeleo ya nchi, jambo linaloendelea kuongeza ari kwa watumishi kutekeleza majukumu yao kwa weledi.
Danda alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika tafiti na sensa mbalimbali zinazofanywa na NBS.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na viongozi wa Serikali na wadau wengine kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa takwimu, ili kuongeza ushiriki wa wananchi na kuhakikisha taarifa zinazokusanywa zinakuwa sahihi na zenye kuakisi hali halisi ya maendeleo nchini.
Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yalianza Juni 28 mwaka huu na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, yakishirikisha taasisi za umma na binafsi zinazowasilisha huduma, bidhaa na ubunifu mbalimbali kwa wananchi.

More Stories
DC awataka viongozi wa serikali za wanafunzi kulinda amani
Usalama waimarisha Mwanza
Hati miliki 527 zakabidhiwa kwa wananchi