Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Mwanza
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa imetoa leseni 16 kwa vyombo vya habari pamoja na mafunzo kwa wadau wa sekta ya utangazaji jijini Mwanza kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu kanuni na masharti ya leseni za maudhui ya utangazaji, sambamba na kuhimiza uzalishaji wa maudhui yanayozingatia sheria, maadili na maslahi ya umma.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Salum,amesema mamlaka hiyo inaendelea kusimamia na kuendeleza sekta ya mawasiliano kwa watoa huduma za utangazaji na wazalishaji wa maudhui ya mtandaoni, kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.
Mhandisi Salum amesema,katika mwaka wa fedha 2025/26, TCRA Kanda ya Ziwa imetoa leseni kwa redio 10 mpya pamoja na mitandao sita ya kijamii, inayozalisha maudhui ya mtandaoni, hatua ambayo imeongeza idadi ya vyombo vinavyofanya kazi katika kanda hiyo.
“Utoaji wa leseni hizi unaonesha kukua kwa sekta ya mawasiliano na kuongezeka kwa ushiriki wa wadau katika utoaji wa taarifa na maudhui kwa umma.Leseni hizo zimeongeza idadi ya redio zilizosajiliwa Kanda ya Ziwa kufikia 59, huku mitandao ya kijamii inayozalisha maudhui ya mtandaoni ikifikia 48,”amesema na kuongeza:
“Tunatoa elimu kwa wadau ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na masharti ya leseni, sambamba na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na zenye manufaa kwa jamii,”.
Mhandisi Salum amefafanua kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwapa wadau uelewa mpana kuhusu wajibu wao wa kisheria, taratibu za utoaji wa leseni na umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma ya utangazaji katika mabadiliko ya teknolojia ya kidijitali.
Aidha,amewataka wamiliki wa vyombo vya utangazaji na wasimamizi wa mitandao ya kijamii kuhakikisha wanazalisha maudhui yenye kujenga jamii, kulinda maslahi ya taifa na kuepuka kusambaza taarifa za upotoshaji au zinazokiuka sheria za nchi.Huku akisisitiza kuwa mamlaka hiyo itaendelea kutoa elimu ili kuhakikisha sekta ya mawasiliano inakua na ikizingatia viwango na matakwa ya kisheria.
Kwa upande wake Ofisa Sheria wa TCRA Kanda ya Ziwa, Joseph Kavishe amesema,mamlaka hiyo imeweka mfumo wa leseni unaolenga kuendeleza sekta ya mawasiliano nchini,ambapo leseni zinazotolewa na TCRA zinahusisha leseni za matumizi ya masafa, leseni za maudhui ya redio na televisheni pamoja na leseni za maudhui ya mtandaoni.
Kavishe amesema mamlaka hiyo inatoa leseni kwa waombaji wapya, kuhuisha muda wa leseni, kufanya marekebisho, kupandisha au kushusha hadhi ya leseni na kufuta leseni pale mmiliki anaposhindwa kutekeleza masharti yaliyowekwa.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Na. 12 ya mwaka 2003, TCRA ina jukumu la kutoa leseni na kudhibiti mifumo ya mawasiliano ya kielektroniki na posta, kuhimiza ushindani wa haki, kulinda maslahi ya watumiaji na kuhakikisha sekta ya mawasiliano inachangia ukuaji wa uchumi wa taifa,”amesema.
Aidha,ameeleza kuwa sekta ya mawasiliano inaendelea kukua kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia, huku huduma na bidhaa mbalimbali za mawasiliano zikiongezeka ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wenye viwango tofauti vya kipato, elimu na maeneo wanayoishi.
“Katika utekelezaji wa majukumu yake, TCRA inashirikiana na wadau wakuu watatu ambao ni Serikali, watoa huduma na watumiaji. Ushirikiano wa makundi haya ndiyo msingi wa mafanikio ya sekta ya mawasiliano,” amesema Kavishe.
Amefafanua kuwa watoa huduma wanahitaji mazingira rafiki ya biashara, utulivu wa kisiasa, usalama wa uwekezaji na fursa za kupata faida kutokana na uwekezaji wao, huku watumiaji wakihitaji huduma bora, za uhakika na zenye gharama nafuu.Hivyo
TCRA inaendelea kusimamia uwiano wa maslahi kati ya makundi hayo ili kuhakikisha maendeleo ya sekta yanaenda sambamba na ulinzi wa haki za watumiaji pamoja na ukuaji wa biashara za mawasiliano.

More Stories
Mix yaendelea kugawa Mamilioni
Katambi atangaza kusitishwa vibali vya mikutano ya Siasa
Uvccm Mtwara yasisitiza Ulinzi wa Amani