*Adai sababu ni uwepo wa dalili za uvunjifu wa amani
Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online-
SERIKALI imeliagiza Jeshi la Polisi kusitisha kwa muda utoaji vibali vya mikutano ya hadhara kwa vyama vyote vya siasa,kwa madai ya kuwepo kwa tishio la machafuko, viashiria vya uvunjifu wa amani na usalama kupitia mikutano hiyo.
Katika ufafanuzi wake, Serikali imesema kumeshuhudiwa mikutano ya hadhara ya baadhi ya vyama vya siasa ikitumika kuhamasisha vurugu na matukio ya uvunjifu wa amani, hali itakayohatarisha usalama wa wananchi.
Hata hivyo, hatua hiyo ya Serikali ni tahadhari ya mapema ili kuepusha kutokea kwa matukio ya uvunjifu wa amani, kama yaliyoshuhudiwa Oktoba 29 na 30, mwaka jana na kusababisha uharibifu wa mali na mauaji ya watu.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi wakati akioa mwongozo kuhusu hali ya usalama nchini kutokana na mipango ya uratibu wa uvunjifu wa amani inayoendelea katika mitandao ya kijamii.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani, ndiyo yenye mamlaka ya kuhakikisha ulinzi wa wananchi na usalama wa nchi na kwa kuwa imeonesha viashiria vya uchochezi, imechukua hatua.
“Kwa sababu uchochezi wa mambo haya umeonekaa dhahiri kwenye maeneo ya kisiasa, namwelekeza IGP Wambura Camillius, asitoe vibali kwa kazi zozote zitakazohusiana na mikutano ya hadhara kipindi hiki kwa chama chochote iwe Chama Cha Mapinduzi, au chama chochote,”amesema.
Pia amesema ni wakati sasa kuwaruhusu wananchi kujenga uchumi wa nchi, kufanya kazi ili kila Mtanzania,wafanyabiashara na wawekezaji watekeleze majukumu yao kwa amani na utulivu.
“Nafanya hivi kwa sababu katika mazingira haya, tukiwatafuta wahalifu ni ngumu kuwachambua katika mkusanyiko wa watu wengi.Wapo ambao wametishia, tumewakamata wengine, wana madumu ya petroli, silaha huku wengine wakipanga uhalifu,”amesema Katambi.
Pia,ameliagiza jeshi hilo kuzifungia baa zote zitakazobainika kutishia uvunjifu wa amani, huku akisisitiza baadhi tayari zimeshafungiwa jijini Dar-es-Salaam.
Viashiria vya uchochezi vinavyoshuhudiwa kutoka kwa baadhi ya wanasiasa hasa wa vyama vya upinzani, ndivyo vile vile vilivyofanywa kabla ya vurugu za Oktoba 29.
Wanasiasa hao, wanatumia majukwaa ya kisiasa kuhamasisha wananchi washiriki matukio hayo ya vurugu na kuhatarisha usalama wa nchi.

More Stories
Vyombo vipya 16 vyapatiwa leseni
Watumishi Rukwa wajengewa uwezo kuhusu Ukimwi na magonjwa yasiyoyakuambukiza
Serikali kuendeleza ujenzi Miundombinu ya Elimu Nanyumbu