*Yaeleza namna tozo za mafuta zinavyoboresha barabara
Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online – Dodoma
BODI ya Mfuko wa Barabara (RFB) imetoa elimu kwa wananchi kuhusu chanzo kikuu cha fedha zinazowezesha matengenezo ya barabara nchini, ikieleza kuwa tozo za mafuta ya petroli na dizeli ndizo msingi mkuu wa upatikanaji wa fedha hizo.
Elimu hiyo imetolewa leo Juni 19,2026kwa wananchi waliotembelea banda la RFB katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Akitoa elimu hiyo kwa wananchi hao katika maadhimisho hayo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara (RFB), Mhandisi Rashid Kalimbaga,amesema mfumo wa tozo za mafuta umewekwa mahsusi kuhakikisha barabara nchini zinaendelea kuwa salama, zenye ubora na zinazopitika kwa urahisi katika misimu yote ya mwaka.
Amesema mbali na mapato yatokanayo na tozo za mafuta, Mfuko wa Barabara pia hupata fedha kupitia tozo zinazolipwa na magari ya kigeni yanayotumia mtandao wa barabara nchini. Kwa mujibu wake, mapato hayo hukusanywa na kuelekezwa moja kwa moja katika kugharamia matengenezo ya barabara za kitaifa na za halmashauri zinazohudumiwa na TANROADS na TARURA.
Mhandisi Kalimbaga ameeleza kuwa uwekezaji katika matengenezo ya barabara una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa kwa kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko, pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.
Ameongeza kuwa kwa sasa Mfuko wa Barabara unafadhili matengenezo ya mtandao wa barabara wenye urefu wa zaidi ya kilomita 181,000 nchini, ambao ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuwezesha shughuli mbalimbali za wananchi katika maeneo tofauti ya Tanzania.
“Kila mchango unaotokana na tozo za mafuta una nafasi muhimu katika kuhakikisha barabara zinaendelea kuwa salama, zenye ubora na zinazoweza kuhudumia mahitaji ya wananchi na uchumi wa taifa kwa ufanisi,”amesema Mhandisi Kalimbaga.
Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea kutembelea banda la RFB katika maadhimisho hayo ili kupata elimu zaidi kuhusu majukumu ya Mfuko wa Barabara, vyanzo vyake vya mapato na namna fedha hizo zinavyotumika kuboresha miundombinu ya barabara kwa manufaa ya Watanzania wote.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu,” ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi kupitia uwajibikaji na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika maendeleo ya taifa.

More Stories
TANESCO yahamasisha matumizi nishati safi
Kihongosi apongeza mradi wa veta Bil 1.6
TBA: Uwajibikaji nguzo ya huduma endelevu