


ce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MENEJA wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) amesema taasisi hiyo inaendelea kuimarisha uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia kaulimbiu ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 isemayo, “Kukuza Uwajibikaji kwa Huduma Endelevu.”
Akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, Mwangosi amesema kuwa TBA ni taasisi ya umma inayotoa huduma mbalimbali kwa wananchi na taasisi za serikali, ikiwemo ushauri wa kitaalamu katika sekta ya ujenzi, ujenzi wa majengo ya serikali, nyumba za watumishi wa umma pamoja na ofisi mbalimbali za umma.
Ameeleza kuwa mbali na majukumu hayo, TBA pia inashiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uwekezaji kwa kushirikiana na sekta binafsi, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mali za umma na kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini.
“Miradi yetu inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na mikoa mingine. Lengo letu ni kuwafahamisha wananchi kuhusu huduma tunazozitoa pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana kupitia TBA,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi kutembelea banda la maonesho la TBA wakati wa maadhimisho hayo ili kupata taarifa sahihi na ufafanuzi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na wakala huo.
“Tunawaalika wananchi wote kutembelea banda letu la maonesho. Timu yetu ipo tayari kuwahudumia na kujibu maswali yote yanayohusu shughuli za TBA pamoja na miradi mbalimbali tunayoitekeleza,” ameongeza.
Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu, amesema TBA inaamini kuwa mafanikio ya taasisi yoyote yanategemea kiwango cha uwajibikaji wa watumishi wake katika kutekeleza majukumu waliyopewa.
“Kila mtumishi amepewa majukumu maalumu ambayo anapaswa kuyatekeleza kwa ufanisi ili kufanikisha malengo ya wakala. Kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu, kila mmoja ana jukumu lake, Wapo wahandisi, madereva, makatibu na watumishi wengine ambao kwa pamoja wanachangia utekelezaji wa malengo ya TBA,” amesema.
Amefafanua kuwa ili kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ufanisi wa kazi, TBA imeendelea kutumia mifumo mbalimbali ya kidijitali inayorahisisha utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Mifumo hiyo ni pamoja na mifumo ya usimamizi wa taarifa za watumishi na mifumo mingine inayosaidia utekelezaji wa majukumu ya kila siku,teknolojia imekuwa nyenzo muhimu katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi ndani ya taasisi,” amesema.
Amesema, TBA pia hutumia mfumo wa upimaji wa utendaji kazi wa watumishi ambapo kila mfanyakazi hupimwa kulingana na majukumu yake na malengo aliyopangiwa.
“Mfumo huu umetengenezwa na wataalamu wa Tanzania na umeongeza uwajibikaji pamoja na ufanisi wa utoaji huduma ikilinganishwa na mifumo iliyotumika hapo awali,” ameeleza.
Vilevile, amesema TBA inaendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wake ili kuongeza ujuzi na uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa viwango vya juu.
“TBA huandaa na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake katika nyanja mbalimbali kulingana na mahitaji ya kazi na maendeleo ya teknolojia,mafunzo hayo yanajumuisha mafunzo ya muda mfupi na ya muda mrefu kwa lengo la kuongeza maarifa, ujuzi na uwezo wa watumishi ili waweze kuendana na mabadiliko yanayotokea katika sekta ya ujenzi na utumishi wa umma kwa ujumla,” amesema.
Amesisitiza kuwa TBA itaendelea kuzingatia misingi ya uwajibikaji, ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma zake, sambamba na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kuchangia maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi.

More Stories
TANESCO yahamasisha matumizi nishati safi
Kihongosi apongeza mradi wa veta Bil 1.6
RFB yatoa elimu kwa wananchi