June 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SELF yatangaza fursa lukuki maonesho wiki Utumishi wa Umma


WANANCHI wa mikoa ya Dodoma na Singida wamehimizwa kutumia fursa ya maonesho ya wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma kutembelea banda la Mfuko wa Fedha ‘SELF Micronance’ na kujifunza kuhusu huduma mbalimbali za mikopo, bima, ujasiriamali na elimu ya fedha zinazolenga kukuza shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha yao.


Mfuko huo, ambao unahudumia mikoa ya Dodoma na Singida kupitia Kanda ya Kati, umeshiriki maonesho hayo kuanzia Juni 16 hadi 23 mwaka huu kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwaeleza fursa zinazopatikana kupitia huduma zake.


Meneja wa SELF Kanda ya Kati, Aristid Tesha, alisema banda la mfuko huo limeendelea kupokea wananchi wengi wanaotafuta taarifa kuhusu mikopo na huduma nyingine zinazotolewa kwa makundi mbalimbali ya jamii.


“Tupo hapa kuwapa wananchi elimu kuhusu ujasiriamali, usimamizi wa fedha na fursa za mikopo zinazotolewa na mfuko wa SELF ili kuwawezesha kukuza shughuli zao za kiuchumi,” ameema Tesha.


Amesema mfuko huo unatoa mikopo kwa wajasiriamali binafsi, watumishi wa umma, wakulima, wafugaji, vikundi vya kijamii, vyama vya ushirika na taasisi ndogo za fedha zinazowahudumia wananchi mijini na vijijini.


Kwa mujibu wa Tesha, miongoni mwa huduma zinazotolewa ni mikopo ya nishati safi inayolenga kusaidia wafanyabiashara wa gesi, vifaa vya umeme na mifumo ya nishati ya jua, huku waombaji wakinufaika na riba nafuu ili kuhamasisha matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira.


Aidha, amesema SELF inatoa mikopo ya kuboresha makazi kwa wananchi wanaohitaji kukamilisha au kukarabati nyumba zao, pamoja na mikopo ya watumishi wa umma inayopatikana kupitia mfumo wa kidijitali.


Tesha alibainisha kuwa mfuko huo pia unatoa mikopo ya jumla kwa vyama vya ushirika na taasisi ndogo za fedha ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wakulima na wafugaji waliopo maeneo ya vijijini.


Mbali na huduma za mikopo, wananchi wanaotembelea banda la SELF wanaweza kupata huduma za bima za vyombo vya moto, nyumba na mali nyingine pamoja na elimu kuhusu umuhimu wa bima katika kulinda uwekezaji na mali zao.


Kwa sasa, SELF ina matawi 12 yanayotoa huduma katika Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini.