Na.Mwandishi wetu,Timesmajira
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kimekutana na wadau kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi katika warsha maalum ya kupitia na kuboresha mitaala tisa ya masomo, hatua inayolenga kuhakikisha programu za mafunzo zinazotolewa chuoni hapo zinaendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira, maendeleo ya teknolojia pamoja na matakwa ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo hapo jana, Mkuu wa Chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga, amesema mapitio hayo ni sehemu ya juhudi za chuo kuhakikisha wahitimu wake wanapata maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji halisi ya waajiri katika mazingira ya sasa yanayobadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Profesa Lwoga amesema CBE imeamua kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kupata maoni yatakayosaidia kuboresha mitaala hiyo na kuifanya iwe na tija zaidi kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
“Tunafanya mapitio ya mitaala yetu ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye. Tunahitaji wahitimu wenye umahiri wa kutosha katika maeneo mbalimbali muhimu ikiwemo matumizi ya akili mnemba (AI), masoko ya kidijitali, usimamizi wa miradi, bima na maeneo mengine yanayoibuka kutokana na mabadiliko ya teknolojia,” amesema Profesa Lwoga.

Ameongeza kuwa ushiriki wa wadau katika mchakato huo ni muhimu kwa kuwa wao ndio watumiaji wakuu wa wahitimu wanaozalishwa na taasisi za elimu ya juu.
“Maoni ya wadau yatatusaidia kubaini maeneo yanayohitaji kuongezewa nguvu na kuhakikisha wahitimu wetu wanakuwa tayari kuingia katika ushindani wa soko la ajira la ndani na kimataifa,” ameongeza.
Kwa upande wao, baadhi ya wadau walioshiriki katika warsha hiyo wamepongeza hatua ya CBE kuwashirikisha katika mapitio ya mitaala, wakisema itasaidia kupunguza changamoto zinazojitokeza kwa baadhi ya wahitimu wanapoingia katika maeneo ya kazi.
Msuluhishi Mkuu wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mwangata Makawa, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kuingiza masuala ya sheria za kazi, usimamizi wa migogoro mahala pa kazi pamoja na maadili ya utumishi katika mitaala ya elimu ili kuwajengea wahitimu uwezo wa kukabiliana na changamoto za mazingira ya kazi.

“Kupitia ushirikishwaji huu wa wadau, taasisi za elimu zinapata nafasi ya kuelewa kwa undani mahitaji ya waajiri. Hii itasaidia kuzalisha wahitimu ambao wataingia moja kwa moja kwenye utekelezaji wa majukumu yao bila kuwa na mapungufu makubwa ya kitaaluma au kiutendaji,” amesema Makawa.
Amesema pia kuwa maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya mifumo ya kazi yanahitaji taasisi za elimu kuendelea kufanya maboresho ya mara kwa mara katika mitaala yao.
“Soko la ajira linaendelea kubadilika kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, hivyo ni muhimu mitaala nayo ikabadilika ili wahitimu waweze kuwa na ushindani na kukidhi matarajio ya waajiri wa sasa na wa baadaye,” amesema
Warsha hiyo imewakutanisha wataalamu kutoka sekta mbalimbali ambao wametoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha ubora wa mitaala ya CBE na kuongeza uwezo wa wahitimu wake kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

More Stories
Aomba kujengewa nyumba,usafiri kwa mjukuu mwenye ulemavu
Historia ya Uhuru wa Tanzania na ukombozi wa Afrika kung’ara Paris
Mwaselela aahidi kumtetea Rais Samia