June 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwaselela aahidi kumtetea Rais Samia


Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MJUMBE wa halmashauri kuu ya taifa ya CCM (MNEC), Ndele Mwaselela amesema ataendelea kumtetea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan usiku na mchana kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika kuwawezesha vijana na watanzania wengi kufikia mafanikio yao.

Mwaselela amesema hayo wakati wa Kongamano la shirikisho la wasomi mkoa wa Mbeya lililofanyika katika ukumbi wa Mkapa, likiwakutanisha wasomi kutoka wilaya mbalimbali kujadili mafanikio na alama za maendeleo chini ya uongozi wa Rais Samia.

“Leo hii tunamfaidi Ndele kwa sababu yupo kiongozi aliyemkuza, aliyemwezesha na kumjengea mazingira ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii. Naye si mwingine bali ni Dkt. Samia Suluhu…..hatuwezi kumlipa kwa fedha, lakini tunaweza kumweleza dunia kwamba Tanzania ina kiongozi bora,” amesema Mwaselela.

Amesema kongamano hilo limeweka historia kwa kuwa miongoni mwa majukwaa yanayojadili kwa kina mafanikio ya Rais Samia na mchango wake katika kuimarisha sekta mbalimbali za maendeleo nchini. Aidha, amesema katika kipindi chake cha uongozi ndani ya MNEC atahakikisha mafanikio ya Serikali yanafika kwa wananchi na kuelezwa kwa lugha rahisi.

Mwaselela amewataka wasomi wa Mkoa wa Mbeya kuendelea kuandaa makongamano katika ngazi za wilaya na kata ili kuwafikia wananchi, hususan wakulima, kwa lengo la kuwaeleza hatua mbalimbali za maendeleo zilizotekelezwa na serikali. Amesema wasomi wanapaswa kutumia elimu yao kuwaelimisha wananchi kuhusu mafanikio ya serikali na fursa zilizopo.

Kwa upande wake, mkuu wa wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, aliyemwakilisha mkuu wa mkoa wa Mbeya, amempongeza Mwaselela kwa ubunifu wa kuanzisha jukwaa hilo la wasomi, akisema limetoa fursa ya kujadili na kuonesha mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia.

Itunda amesema mkoa wa Mbeya umeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato kwa kuvuka asilimia 100 ya malengo kabla ya Juni 30 mwaka huu wa fedha. Ameongeza kuwa vijiji vyote 333 vya mkoa huo tayari vimeunganishwa na huduma ya umeme, huku vitongoji 1,880 kati ya 2,951 vikifikishiwa huduma hiyo.

Naye mkazi wa Sinde, Zawadi Juma, amesema wananchi wameona juhudi kubwa za Rais Samia katika sekta za elimu, maji na miundombinu ya barabara. Ameongeza kuwa Mwaselela amekuwa nguzo muhimu kwa Mkoa wa Mbeya katika kueleza na kutangaza mafanikio ya Rais kwa wananchi.