*Milioni 460 kusambaza majiko hayo kwa wananchi 6,488.
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Mbozi.
SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na kampuni ya ECOMAMA ICS Technology,imezindua mradi wa usambazaji majiko banifu mkoani Songwe,wenye thamani ya shilingi milioni 463.8.
Mradi huo unaolenga kuwasaidia wananchi kupata nishati safi na salama ya kupikia kwa bei nafuu umezinduzi Juni 10,2026 wilayani Mbozi, ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Hamad Mbega,ambaye amewataka wananchi, hasa akina mama, kuchangamkia fursa hiyo adhimu.

Mbega ametoa rai kwa viongozi wa REA kuongeza idadi ya majiko hayo kutokana na idadi kubwa ya watu,ambapo amesema katika Mkoa wa Songwe una wakazi takribani milioni 1.3, huku nusu yao wanaishi wilayani Mbozi na wengi wao wana mwamko mkubwa wa kutumia nishati safi.
Kwa upande wake Meneja wa Miradi ya Nishati Safi Mkoa wa Songwe, Vencha Maganga amesema, Mkoa huo umepata mgao wa majiko 6,488 ambapo kiasi cha shilingi milioni 463.892 zimetengwa kwa ajili ya zoezi hilo la usambazaji wa majiko hayo kwa njia ya ruzuku ambapo kila Wilaya itapata majiko 1,622 yenye thamani ya shilingi milioni 115.973.
Maganga amezitaja Wilaya zitakazonufaika na mgao huo ni nne ambazo ni Wilaya ya Mbozi,Momba,Songwe na Ileje.
“Ugawaji huu ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuondoa matumizi ya nishati zisizo safi na salama nchini pamoja na kulinda mazingira.Natoa wito kwa wananchi wote, hususani wakina mama kuchangamkia fursa hii ya majiko banifu ambayo kabla ya Serikali kutoa ruzuku,walipaswa kuyanunua kwa sh. 71,500 lakini sasa imelipa sh. 57,200 sawa na asilimia 80,”amesema Maganga.
Mkurugenzi wa Kampuni ya ECOMAMA, Sabitina Makweta, amewahakikishia wananchi kuwa majiko hayo ni salama na yamethibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Aidha, Makweta alitaja sifa za majiko hayo kuwa ni ubanaji wa matumizi,yanatumia kuni mbadala kidogo na mkaa mbadala mchache na pia ni rafiki kwa mazingira na yanaruhusu hewa safi ya oksijeni kupita kwa urahisi

.


More Stories
Mapato ya Ndani yaimarisha Bajeti ya Serikali
Salome:Ushirikiano wa wadau ni muhimu kufikia lengo la Nishati Safi ya Kupikia
Wazalishaji teknolojia nishati safi watakiwa kufuata viwango