Na Mwandishi Wetu-Timesmajira Online-Muleba
MASHINDANO ya Mwijage Cup uliofanyika yamezinduliwa rasmi huku timu 20 za ndondo kutoka Tarafa ya Kamachumu wilayani Muleba mkoani Kagera,zikitarajia kuchuana.
Mashindano hayo ambayo yanalenga kuwasaidia vijana kuwa na uwezo wa kucheza mpira wenye viwango vya kimataifa,kuinua vipaji na kutengeneza vipaji vipya kwenye mpira wa miguu kutoka ngazi za chini watakaokwenda kucheza kwenye timu kubwa za kitaifa na kimataifa.

‎
‎Akizungumza katika uzinduzi uliofanyika Juni 7,2026,katika uwanja wa mpira wa Polisi Kamachumu uliopo Kata ya Kamachumu wilayani Muleba mkoani Kagera,Msemaji wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally,amemuomba muandaaji wa mashindano hayo,kuyafanya yawe endelevu kwa lengo la kuibua vipaji kuliko kusubiri muda wa kuomba kura au jambo fulani linalohusu maslahi binafsi.
Amesisitiza kualika watu wenye maamuzi katika ligi hiyo wakati ikiendelea ili wafanye usajili wa vijana kutoka maeneo mbalimbali pamoja na kushirikisha wataalamu ambao wamesomea mpira ili waweze kupata wachezaji kutoka ngazi ya chini.
“Haya mashindano siyo ya kubeza yanaibua vipaji ambavyo sisi tulioko huku juu hatuwezi kuvigundua,mfano sisi Simba tuliwahi kupata mchezaji mzuri aitwaye Seleman Mwalimu ambaye alianza kucheza mpira kutoka kwenye timu ndogo za ndondo wilayani Hai kule mkoani Kilimanjaro,huku chini kuna vipaji,”amesema Ally.
Amesema, amefurahi kufika Kamachumu na kukutana na wanachama wa Simba na wapenda michezo, “Nimeona kuna mwamko mkubwa wa michezo hasa mpira wa miguu, tumuunge mkono mwanzilishi wa mashindano haya ambaye amewafanya vijana kuonekana kupitia vipaji vyao vya mpira,”.

Mdhamini na muandaaji wa mashindano hayo Paul Mwijage,amesema, lengo la mashindano hayo ni kukuza vipaji vya vijana ambao wanateketea kwa ulevi,madawa ya kulevya,yatima wasio na msaada.Ambapo kupitia mashindano ya mpira wa miguu wataweza kuyatumia kama fursa kujiinua katika masuala mbalimbali kwa kutumia vipaji vyao.
‎
‎”Lengo la kuwekeza nyumbani kwa kuanzisha ligi hii, ni kukuza vipaji vya michezo kwa vijana wengi wanaopoteza matumaini katika soka, tumelenga kusaidia kukuza soka la Tarafa ya Kamachumu,wilaya ya Muleba,Mkoa na Taifa kwa ujumla,ndiyo maana tumemleta Msemaji wa Simba Ahmed Ally ili na yeye aone kuwa hata vijijini kuna vipaji vya mpira kutoka kwa vijana wetu,”amesema Mwijage.
Kwa upande wake Ofisa Michezo na Utamaduni wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Denis Joseph amesema,Serikali inawaunga mkono wale wote wenye nia ya kuanzisha ligi kama hizo,hivyo wasisite ili waibue vipaji na kupata wachezaji wazuri ambao ni alama ya kuitangaza Wilaya hiyo ndani na nje ya nchi.
Nahodha wa timu ya Bafanabafana inayoshiriki mashindano hayo Anick Ansberth,amesema malengo na matarajio yake kupitia mechi za ndondo zitamsaidia kujulikana na timu kubwa au kujiunga na vituo vya michezo,zitakazo wasaidia kuwa wachezaji wazuri na bora kwa sababu wao bado ni vijana wadogo ili baadae waweze kucheza katika timu kubwa.
Ansberth,anasema katika mashindano hayo anajifunza nidhamu na utulivu uwanjani ili aweze kufanikiwa kufikia malengo yake ya kuwa mchezaji bora wa kutumainiwa katika timu kubwa atakayofanikiwa kuichezea.



More Stories
Mixx yajivunia ongezeko la Wateja kupitia kampeni yake
Airtel,Serikali waungana kupanda miti Bagamoyo na kusafisha fukwe Dar
NBS: Takwimu Muhimu Kufanikisha Dira ya Taifa 2050