Na Joyce Kasiki, Timemajira Online, Dodoma
NAIBU Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, ameipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa mchango wake mkubwa katika utoaji wa huduma za utabiri wa hali ya hewa zinazosaidia wananchi kupanga shughuli mbalimbali za maendeleo na kuhifadhi mazingira.
Kwagilwa alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la TMA katika maonyesho ya Wiki ya Mazingira Duniani yalianza Juni Mosi na kutarajiwa kuhitimishwa Juni 5 mwaka huu katika viwanja vya Jakaya Kikwete jijini Dodoma .
Akiwa katika banda hilo, alipata fursa ya kufahamishwa huduma mbalimbali zinazotolewa na TMA pamoja na mchango wake katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi mazingira.
Akizungumza katika banda hilo , Mtaalam wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Daniel Masunga, amesema mamlaka hiyo inaendelea kuhakikisha wananchi wanaopata taarifa za hali ya hewa wanaongezeka ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi katika shughuli zao za kila siku.
“Wananchi ambao wanategemea taarifa za hali ya hewa kwa shughuli zao, hususan kilimo, wanapaswa kuzipata taarifa hizo kwa wakati na kwa urahisi zaidi, hasa waliopo vijijini. Tunahakikisha wananchi wote wanapata taarifa za utabiri wa hali ya hewa kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla,” amesema Masunga.
Amesema kuwa TMA inatoa huduma mbalimbali za hali ya hewa zinazowasaidia watu kupanga na kutekeleza shughuli rafiki kwa mazingira pamoja na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Masunga amesema pia mamlaka hiyo hutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa mapema ili kuwezesha wananchi, serikali, sekta binafsi na wadau wengine kuchukua hatua stahiki za kujikinga dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza.
“Tunatoa tahadhari kwa wakati kuhusu hali mbaya ya hewa inayotarajiwa kutokea ili watu binafsi, taasisi na serikali waweze kuchukua hatua za mapema na hivyo kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na hali hiyo,” amesema.
Ameongeza kuwa TMA pia hutoa huduma maalumu za utabiri kulingana na mahitaji ya wateja katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, madini, usafiri wa anga pamoja na sekta nyingine za kiuchumi.
“Wakati mwingine hata waandaaji wa michezo huhitaji utabiri mahsusi wa hali ya hewa katika maeneo maalumu kama viwanja vya michezo. Tuna uwezo wa kutoa utabiri wa maeneo makubwa na madogo kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali,” amefafanua.
Kwa mujibu wa Masunga, Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika rasilimali watu, miundombinu, vifaa na teknolojia za kisasa zilizoiwezesha TMA kufikia usahihi wa zaidi ya asilimia 90 katika utabiri wa hali ya hewa.
“Kwa sasa utabiri wetu una usahihi wa zaidi ya asilimia 90,kutokana na maendeleo hayo, wananchi wengi wameacha kutumia kauli kwamba hali ya hewa haitabiriki, kwa sababu sasa hali ya hewa inatabirika kwa kiwango kikubwa na kwa uhakika zaidi,” amesema.

More Stories
DCEA, VETA kuwapa ujuzi warahibu dawa za kulevya
Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya familia
Kihongosi ahimiza ulipaji ada ya uanachama