June 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC,Chirukile ziarani Kongo kujenga mahusiano ya Kidiplomasia,uchumi

Na Israel Mwaisaka

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Ally Chirukile, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Charles Makongoro Nyerere, ameendelea kuifungua Rukwa katika jukwaa la Kimataifa baada ya kufanya ziara rasmi katika Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambako amekutana na kutoa salamu kwa Balozi wa Tanzania Nchini humo, Said Juma Mshana.

Ziara hiyo ya Ubalozini aliyoifanya Mei 30, 2026 Jijini Kinshasa imekuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia, biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na DRC, Mataifa ambayo yanaendelea kunufaika na ushirikiano wa kiuchumi unaokua kwa kasi katika ukanda wa Maziwa Makuu.

Mbali na kutembelea Ubalozi wa Tanzania, Chirukile amefika katika tawi la CRDB Bank Mjini Kinshasa kujionea huduma zinazotolewa na taasisi hiyo ya kifedha katika kurahisisha miamala ya biashara kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na DRC.

Ameeleza kuwa uwepo wa huduma za kisasa za kibenki unasaidia kupunguza changamoto za usafirishaji wa fedha taslimu na kuongeza usalama wa miamala ya kibiashara, hali inayochochea ukuaji wa biashara na uwekezaji kati ya Nchi hizi mbili.

“Kuimarika kwa huduma za kifedha za kuvuka mipaka ni msingi muhimu wa kukuza biashara, kuongeza uwekezaji na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wetu,” amesema Chirukile.

Ziara hiyo imefanyika baada ya Chirukile kumuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, katika maonesho makubwa ya biashara ya ExpoBeton yaliyofanyika Kalemie, Jimbo la Tanganyika nchini DRC. Maonesho hayo yamekusanya viongozi wa Serikali, wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Mataifa mbalimbali kwa lengo la kutangaza fursa za biashara, uwekezaji na maendeleo ya miundombinu.

Akizungumzia umuhimu wa ushiriki wa Mkoa wa Rukwa katika maonesho hayo, Chirukile amesema Mkoa wa Tanganyika una umuhimu mkubwa kwa Tanzania kutokana na ukaribu wake na mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa kupitia Ziwa Tanganyika, jambo linalofungua milango ya usafirishaji, biashara ya mipakani na ushirikiano wa kiuchumi unaowanufaisha wananchi wa pande zote mbili.

Amebainisha kuwa kupitia ExpoBeton, fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta za biashara, usafirishaji, kilimo, viwanda na huduma zimeendelea kutangazwa, hatua inayotarajiwa kuongeza mtiririko wa bidhaa na huduma kati ya Tanzania na DRC.

Wadau wa biashara wanaeleza kuwa kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na DRC kunatoa nafasi kubwa kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Rukwa kutumia ukaribu wa kijiografia wa Ziwa Tanganyika kupanua masoko ya bidhaa na huduma zao katika soko la DRC lenye mamilioni ya watumiaji.

Ziara hii imeendelea kuonesha namna viongozi wa Serikali wanavyotumia majukwaa ya Kimataifa kutangaza fursa za Tanzania, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya uchumi wa Nchi.