May 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CAMFED Ilivyobadili maisha ya wasichana Tanzania

Na  Mwandishi wetu 

AKIWA  mwanafunzi wa kidato cha tatu, na umri wa miaka 18  tu wakati huo,Tatu Limage alijikuta akibeba jukumu  la kulea wa wadogo zake wawili baada ya familia yao kukumbwa na changamoto za maisha.

 Leo, akiwa na umri wa miaka 30, ameandika historia mpya kwa kuanzisha kituo cha kulelea na kufundisha watoto kinachomuingizia mamilioni ya shilingi.

Safari yake ya mafanikio ni ushahidi namna shirika la CAMFED, linavyowezesha wasichana na wanawake vijana kuvunja mzunguko wa umaskini kupitia elimu, uongozi na ujasiriamali.

Maisha ya utotoni yenye changamoto

“Tuliishi kwa kula mlo mmoja kwa siku. Mara nyingi tulikwenda shule bila kifungua kinywa,” anasimulia Limage kwa hisia huku akitokwa na machozi.

Baada ya wazazi wake kutengana, alibaki akiwalea wadogo zake wawili kama mama yao,hata hivyo baada ya kumaliza kidato cha nne katika shule ya sekondari  Sanje, alishindwa wa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita.

Mwaka 2015 alikaa nyumbani, na baadaye akaanza kuuza vitumbua katika ofisi mbalimbali ili kujipatia kipato.

Kutoka muuzaji vitumbua hadi mwalimu

Mwaka 2017, Limage alijiunga na mafunzo ya miezi sita ya elimu ya awali, kisha akapata kazi ya kufundisha katika shule binafsi.

Mwaka 2018, alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Tandala (Tandala Teachers College) kilichopo mkoani Njombe na kuhitimu mwaka 2020.

Baada ya kurejea  jijini Dar-es-Salaam, alifahamishwa kuwa shirika la CAMFED ilikuwa ikiendesha programu za kuwajengea uwezo wanawake vijana, jambo lililompa fursa ya kujitolea kuwafundisha watoto wa kike kuhusu kujitambua, kujiamini na kupanga maisha yao.

Kuanzisha ‘Talima Day Care’

Mwaka 2022,Limage alianza kituo chake cha kulea watoto mchana cha Talima kikiwa na watoto wawili tu huku akiendelea kufundisha shule nyingine.

Safari ya kuanzisha kituo hicho haikuwa nyepesi kwani alitumia sehemu ya  mshahara wake wa sh.150,000 kwa mwezi kulipia kodi ya sh.60,000 ya chumba alichotumia kufundishia.

Hatua kwa hatua, wazazi walianza kuelewa dhamira yake,idadi ya watoto ikaongezeka kutoka wawili hadi 10 na kisha kufikia  50.Leo  kituo chake cha Talima Day Care kina watoto 105 waliosajiliwa, wakiwemo wasichana 45 na wavulana 60.

CAMFED yatoa mkono wa kuwezesha

Mwaka 2024, Limage alipata mkopo wa kwanza kutoka shirika la CAMFED uliomwezesha kuhamia katika jengo kubwa zaidi na baadaye alipatiwa kiasi cha  sh.500,000 kwa ajili ya  kuboresha mazingira ya kujifunzia ikiwemo kupaka rangi 

Ndani ya mwaka huo huo, alipata mkopo mwingine wa  sh.milioni 2 na kuurejesha kwa mafanikio,jambo lilofanya shirika hilo kuendelea kumwamini na kuona ni binti mpambanaji anayepaswa kushikwa mkono.

Mwaka 2025, baada ya mwenye nyumba kutangaza kuuza jengo alilokuwa akitumia,Limage aliomba msaada tena kwa shirika hilo  na kupatiwa mkopo wa sh  milioni 50.

“Nilijikuta najiuliza kama kweli ni mimi au ninaota. Nilimlipa mwenye nyumba sh.milioni 25 na fedha iliyobaki nikafanya ukarabati mwa ‘Talima Day Care,’” anasema.

Maono ya kubadili jamii

Mbali na mafanikio ya kifedha, Limage anasema lengo lake kuu ni kuwasaidia watoto kupata malezi bora, kujifunza katika mazingira salama na kuepuka kuzurura mitaani.

Zuberi Ungando anasema tangu kuanzishwa kwa kituo hicho, uzururaji  na matukio ya kupotea kwa watoto yamepungua kwa kiasi kikubwa katika eneo hilo.

Mwanachuo aliyerejea masomoni baada ya kujifungua

Hadithi ya Mwanne Said inaonesha upande mwingine wa mafanikio yanayochochewa na shirika la CAMFED.

Akiwa mwanafunzi wa kidato cha tatu, alipata ujauzito na kukatishwa tamaa na familia yake, hata hivy baada ya Serikali kuruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kurejea shule, alifanikiwa kurejea shuleni kupitia kudhamini wa shirika la CAMFED.

Leo,Said ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Tumaini University Dar-es-Salaam akigharamiwa ada, matibabu, usafiri na mahitaji mengine yote muhimu.

“Sitawalipa kwa fedha, bali kwa kujituma katika masomo na kuwa mfano kwa jamii,”anasema Said.

Wito kwa wasichana 

Said  anawahimiza wasichana kutokata tamaa wanapokumbana na changamoto za kimaisha anasema,“Ukikosea, unaweza kusamehewa,ukijituma, unaweza kusonga mbele na kutimiza ndoto zako,”.

Ana ndoto ya kuanzisha kampuni yake mwenyewe baada ya kuhitimu masomo ya biashara na kutoa ajira kwa vijana wengine.

CAMFED na safari ya kubadili historia ya wasichana 

CAMFED limekuwa shirika la kimataifa linalosaidia wasichana kutoka mazingira magumu kupata elimu na kuwa viongozi wa mabadiliko katika jamii zao.

Kupitia mikopo, udhamini wa masomo, mafunzo ya ujasiriamali na uongozi, shirika hilo limeendelea kubadili maisha ya maelfu ya wasichana nchini Tanzania na barani Afrika.

Hata hivyo kwa Tatu Limage na Mwanne Said, CAMFED si shirika la kawaida ni daraja lililowavusha kutoka maisha ya changamoto hadi mafanikio.