Na Penina Malundo,Timesmajira
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari pamoja na Mwanariadha nyota wa Tanzania, Alphonce Simbu wanatarajiwa kushiriki katika mbio za Wakili Marathon 2026 zitakazofanyika Mei 31, 2026 katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma kwa lengo la kuhamasisha utoaji wa msaada wa kisheria kwa jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) na waandaaji wa mbio hizo, Ado November amesema maandalizi yote ya mashindano hayo yamekamilika na kwamba mbio hizo zina hadhi ya kimataifa kutokana na kuzingatia vigezo vinavyotakiwa.
Amesema waandaaji wanatarajia kupokea zaidi ya washiriki 5,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini, huku akiwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mashindano hayo yatakayokuwa pia na vipengele vya burudani na shughuli za kijamii.
“Tumewaandalia wananchi mbio za viwango vya kimataifa na tunatarajia washiriki zaidi ya 5,000. Hii ni fursa muhimu ya kuhamasisha utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi,” amesema Ado November.
Amefafanua kuwa gharama za ushiriki zitakuwa kati ya Sh40,000 na Sh150,000 kulingana na kategori mbalimbali za washiriki, huku washindi wakitarajiwa kujinyakulia medali pamoja na zawadi tofauti.
Mbali na mbio za watu wazima, amesema kutakuwa pia na mbio maalum kwa watoto sambamba na matukio ya burudani yatakayowakutanisha wasanii pamoja na viongozi mbalimbali wa kitaifa.
Ado amesema kupitia Wakili Marathon 2026 wataendelea kusaidia jamii kwa kutoa huduma za msaada wa kisheria bure, akibainisha kuwa hadi sasa zaidi ya Watanzania milioni nne katika mikoa nane tayari wamefikiwa na huduma hiyo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Rais wa Chama cha Riadha Tanzania (RT) na mwanariadha nguli wa Tanzania, Juma Ikangaa amesema mbio hizo pia zitakuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vipya vya riadha vitakavyosaidia kupata wanariadha wengine watakaoiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
Aidha, Ikangaa amepongeza PBA kwa kufanikisha maandalizi yanayokidhi viwango vya kimataifa vya mashindano hayo, huku akisisitiza kuwa RT itaendelea kushirikiana na waandaaji kuhakikisha vipaji vya wanariadha chipukizi vinaendelezwa nchini.

More Stories
Madaktari Mloganzila wanufaika na mafunzo maalum ya tiba za mifupa
CCM yatoa salamu nzito kwa Samia-Butiama
Waziri wa Fedha aipa kongole CRDB