Na Judith Ferdinand,Mwanza
KAMPENI ya utoaji chanjo ya polio kwa njia ya matone awamu ya pili kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 10, imekamilika Mei 10,2026, huku Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza ikifanikiwa kuvuka lengo kwa asilimia 103.
Ambapo halmshauri hiyo ilifanikiwa kuwachanja jumla ya watoto 181,178, huku lengo likiwa ni kuwafikia watoto 174,644.
Kampeni hiyo ambayo imefanyika kwa Mikoa saba ikiwemo Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu,Mara,Tabora na Singida kwa siku nne kuanzia Mei 7 -10,2026,ni jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Afya kuwakinga watoto na virusi hatari vienezavyo ugonjwa wa polio.
Akizungumza jana,Mratibu wa Chanjo wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Shamte Almasi amesema, baada ya kutolewa kwa chanjo hiyo ya polio aina ya noVP2,anaamini kuwa watoto sasa wako salama.
Shamte ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wazazi kuwa na mwamko wa kuwapatia watoto wao chanjo mbalimbali kama ilivyokua kwenye chanjo hiyo,ili kuweza kuwakinga na maradhi mbalimbali.
Muuguzi na Mratibu wa Chanjo Kituo cha Afya Buzuruga,Damarice Dawson amesema,muitikio umekua mkubwa kwa wazazi kuwaleta watoto wao kupata chanjo hiyo,hivyo aliwapongeza kwa ushirikiano waliouonesha katika kipindi chote cha kampeni.
Kwa upande wake Furaha Mwita mkazi wa Kata ya Buzuruga,amesema anafuraha watoto wake wamepata chanjo hiyo,hivyo anaamini watakuwa salama.
Naye Majani Maharage mkazi wa Buzuruga,amesema ni mara ya kwanza kumpeleka mtoto wake  kupata chanjo ya polio ambayo ni nzuri kwa afya ya watoto huku akiwasisitiza wazazi wengine kushiriki kampeni kama hizo.
“Tumeletewa chanjo bure hakuna gharama yoyote.Chanjo ni nzuri na haina madhara yoyote,”amesema Mwanne Ally mkazi wa mtaa wa Buzuruga Kusini.

More Stories
Kortini kwa kujifanya afisa wa Magereza na kuomba rushwa
Wanaodai fidia walipwe ndani ya miezi mitatu
Serikali kuimarisha Utendaji wa TPHPA