May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi watakiwa kuondoa unyanyasaji wananchi

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

VIONGOZI wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza wametakiwa kusimamia nidhamu kwa askari ili kuondoa vitendo vya  unyanyasaji  kwa wananchi.

Huku jeshi hilo likitakiwa kuendelee kuimarisha Kamisheni ya  Polisi Jamii kwa kupeleka wakaguzi kwa kila kata ili kuongeza ufanisi wa kazi za ulinzi na usalama pamoja na  kuendelea  kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, uhalifu wa mitandaoni na kuimarisha kitengo cha intelijensia kwa kutumia mifumo ya kisasa ya teknolojia.

Hayo yameelezwa Mei 9,2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda wakati wa maadhimisho ya Siku ya Familia ya Polisi(Police Family Day) kwa Mkoa huo yaliofanyika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

“Tunapoendelea kujivunia Tanzania kuwa kisiwa cha amani, tunathamini mchango wa Jeshi la Polisi. Ni muhimu kusimamia nidhamu kwa askari ili kuondoa matumizi mabaya ya madaraka, vitendo vya kuonea na kunyanyasa wananchi,”amesema Mtanda.

Mtanda amesema,jeshi hilo ni  mali ya wananchi na si la viongozi.Hivyo wananchi wanapaswa kuridhishwa na utendaji  kazi wake.

“Maofisa na askari wasio waadilifu waache tabia hizo. Hatutaki kuona wananchi wakichonganishwa na polisi. Jeshi lina miiko, maadili na taratibu zake, hivyo kila mmoja azingatie sheria na kanuni za kazi,”amesema Mtanda.

Sanjari na hayo,Mtanda amewataka maofisa na askari wa jeshi hilo,kuwa kielelezo cha taswira nzuri mbele ya jamii kwa kuzingatia misingi ya upendo, haki na kuheshimiana katika utendaji wao wa kazi zikiwemo familia zao na  kuepuka mienendo isiyofaa.

“Upendo ukikosekana hata kazi haziwezi kufanyika kwa ufanisi. Wakubwa wasiowaonee wadogo, bali tuimarishe mshikamano na ushirikiano mahali pa kazi ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi,”amesema Mtanda.

Katika jitihada za kupambana na umasikini miongoni mwa askari,amewahamasisha kutumia fursa za mikopo yenye riba nafuu kupitia Ushirika wa Akiba na Mikopo wa Usalama wa Raia (URA Saccos) ili kuongeza vipato vyao badala ya kuwaonea wananchi.

Kwa upande wake, Nabii Mchungaji B.G. Malisa,amesema, msingi wa amani ni upendo na haki,ambao huvumilia na husamehe,hivyo licha ya  polisi  kuhakikisha wananchi wanakuwa salama ni muhimu kuendelea kujenga upendo na mshikamano katika jamii.

Akinukuu maandiko matakatifu  kutoka kitabu cha Mathayo 24:12,Malisa amesema,”Kwa sababu ya maasi kuongezeka, upendo wa wengi utapoa.Upendo huvumilia, hauhesabu mabaya na unasamehe”.