May 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani Lushoto wataka fedha kutengeneza barabara

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOline,Lushoto

BAADHI ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wamesema wapeleke ombi maalumu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili waweze kupewa fedha za kukarabati miundombinu ya barabara iliyoharibika kwa mvua zinazonyesha.

Wamesema kuharibika kwa miundombinu ya barabara kumeharibu uchumi wa wakulima, wafanyabiashara na mapato ya halmashauri, kwani magari yameshindwa kufika vijijini kuchukua mazao ya wakulima, mbao, mbogamboga na matunda sababu barabara zimeharibika.

Waliyasema hayo Mei 5, 2026 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo wakati wanachangia taarifa ya Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Richard Gama.

“Madiwani wakiwa kikaoni.”

Diwani wa Kata ya Mbaramo, Hatibu Ulanga ambaye amekuwa diwani kwa zaidi ya miaka 25 sasa, alisema siku za nyuma walipokutana na changamoto kubwa kama hiyo, waliomba mafungu ya fedha ya dharura ili kuweza kuzifanyia ukarabati barabara zilizoathirika.

“Kutokana na tatizo kubwa lililotukuta la kuharibika kwa barabara nyingi za vijijini tunatakiwa tuombe fedha kupitia fungu maalumu serikalini ili kufanyia ukarabati barabara zetu. Na hilo hatukuanza leo, siku za nyuma tulipokutana na changamoto hii, tuliomba fungu maalumu la fedha kwa ajili ya kufanyia matengenezi ya barabara zetu,”amesema Ulanga.

Diwani wa Kata ya Shume Elias Kivatiro amesema kwenye kata yake halmashauri imepata hasara ya zaidi ya sh. milioni 10 sababu barabara ya Viti- Gologolo ya kilomita 10 haipitiki, na barabara hiyo ni muhimu kwa ajili ya magari yanayokwenda kuchukua mbao na mbogamboga.

“Kwenye kata yangu ya Shume halmashauri imepata hasara ya zaidi ya sh. milioni 10 sababu magari hayafiki na wengine wameegesha vijijini, hivyo Serikali kushindwa kukusanya ushuru na tozo mbalimbali za mazao ya misitu kutoka Shamba la Miti Shume kama vile mbao. Pia kwa magari ynayobeba mbogamboga, hivyo wakulima na wafanyabiashara wameathirika kwa mazao yao kushindwa kusafirishwa kwa wakati,”amesema Kivatiro.

“Diwani wa Kata ya Mbaramo, Hatibu Ulanga”

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Dkt. Ikupa Mwasyoge amewahimiza madiwani kwenda kuwahamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, kwani itawasaidia kupata matibabu kwa uhakika kaya ya watu sita.

“Mwananchi asisubiri ameugua, kwani ni vizuri kujiandikisha mapema, na kwa kaya ni sh. 150,000, yaani inakuwa ni baba, mama na watoto wanne wasiozidi miaka 21, na matibabu yanaanza baada ya miezi mitatu. Kwa hiyo niwaombe madiwani muende mkatoe elimu na kuwahamasisha wananchi kuweza kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote,”amesema Dkt. Mwasyoge.

“Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Whitney Mwizagi akifunga Baraza.”

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Whitney Mwizagi amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuwapatia sh. milioni 900.3, ambapo kati ya fedha hizo, sh. milioni 100 ni kwa ajili uboreshaji wa masoko na magulio, sh. milioni 500 kwa ajili ya ukarabati wa Ofisi Kuu ya Halmashauri pamoja na samani, hasa kuweka samani mpya Ukumbi wa Mikutano (Baraza la Madiwani), na sh. milioni 249 kwa ajili ya ujenzi wa uzio nyumba za Wakuu wa Idara.

Mwizagi pia aliwasisitiza madiwani kwenda kuhimiza ukusanyaji wa mapato ya halmashauri, kwani mapato ndiyo uti wa mgongo wa halmashauri hiyo ili iweze kutoa huduma za kijamii na kiuchumi.

“Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Dkt. Ikupa Mwasyoge.”
“Diwani wa Kata ya Shume Elias Kivatiro (kulia).”
“Wakuu wa Idadi na Vitengo, vyama vya siasa, maofisa tarafa na waalikwa wengine wakifuatilia kikao cha Baraza.”