Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOline,Lushoto
WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Lushoto wamesema Mradi wa Maji Lushoto mjini upo kwenye hatua za mwisho kukamilika baada ya Serikali kumlipa Mkandarasi sh.mil. 260.3 ili aweze kukamilisha mradi huo unaotarajiwa kukamilika Juni 25, 2026.
Hayo yamesemwa Mei 5, 2026 na mwakikishi wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto, Fredy Mbulumi kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, huku akielezea miradi ya maji inayoendelea kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto:

“Mkandarasi ameshalipwa IPC Na 3 ya sh. mililioni 260.3. Ameshaleta bomba kwa ajili ya kumalizia eneo la ulazaji bomba kwenye njia kuu ya bomba (Gravity Main). Kwa sasa mkandarasi yupo site anaendelea na kazi ya kuseti bomba kwenye laini ya bomba kuu. Kulingana na muda alioongezewa wa kazi ni mategemeo ifikapo Juni 25, 2026 kuwa mradi uwe umeshakamilika,”amesema Mbulumi.
Mbulumi amesema ukarabati wa Mradi wa Maji Gologolo/Hemtoye, Mkandarasi ameshalipwa hati yake ya malipo na kwa sasa yupo eneo la kazi gologolo, anaendelea na kazi ya ulazaji bomba na ujenzi wa vituo vya maji (DPs).
Mwingine ni Mradi wa Maji Bungoi- Kwemshasha, Mkandarasi yupo kazini na anaendelea na ujenzi wa Jengo la Ofisi ya CBWSO katika Kijiji cha Mwangoi.

Mbulumi amesema mwingine ni ujenzi wa Mradi wa Maji Mkundiambaru na Mkundiamtae. Mradi huo umeshakamilika na unatoa huduma ya maji katika Kijiji cha Mkundiambaru na Mkundiamtae.
“Changamoto zinazoathiri huduma ya maji ni wananchi kuhujumu miundominu ya maji kwa kukata mabomba hususani wananchi wa Kijiji cha Mkundiambaru. uharibifu wa ukataji miundombinu una athari mbaya katika utoaji wa huduma, ambapo kwa sasa mradi upo katika kipindi cha uangalizi,”amesema Mbulumi.


More Stories
Madiwani Lushoto wataka fedha kutengeneza barabara
Mbunge Arumeru Magharibi aomba Kiwanja cha Mpira jimboni
Yas, yaendesha kambi huduma za macho bure Kilwa