May 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kihongosi:CCM tunaamini katika maridhiano

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dodoma.

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amesema chama hicho kinaamini katika maridhiano, huku kikiamini kuwa njia hiyo ni moja ya nguzo ya amani nchini pamoja na kupunguza migogoro.

Kihongosi ameyasema hayo Mei 4, 2026 jijini Dodoma, alipokuwa akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari, akisema kuwa, siyo mara ya kwanza katika nchi kufanyika maridhiano.

“CCM kama chama tunaamini katika maridhiano na maridhiano haya si ya kwanza kufanyika au kutokea katika nchi yetu. Katika nyakati ambapo kelele au tofauti ya kisiasa katika jamii au itikadi zinapoongezeka, jambo moja linabaki kuwa la msingi kuliko yote ni hatma ya Taifa haiwezi kujengwa juu ya misimamo mikali bali juu ya uwezo wa kukaa pamoja na kusikilizana.

“Chama cha Mapinduzi kinaamini pale mazungumzo yanapopewa nafasi migogoro inapungua, taasisi zinaimarika na maendeleo yanapata mizizi imara hasa katika kuwatumikia wananchi,”amesema Kihongosi.

Amesema, chama kinatoa wito wa kushirikisha makundi yote yakiwemo vyama vya siasa, viongozi wa dini, asasi za kiraia, vyama vya wafanyakazi, sekta binafsi, viongozi wa kimila, wananchi na wadau wa maendeleo ili kuwepo na maridhiano.

“Watu wanaamini kwamba maridhiano ni baina ya vyama vya siasa..hapana ni mambo yanayohitajika kuzungumzwa kwa upana wake na nchi yetu ina vyama zaidi ya 18 maana yake vyama hivyo vinauwezo wa kushiriki kuridhiana katika maeneo ambayo tunaona yana msingi huo.

“Tunasema hivyo tukitambua kuwa siyo wadau wa pembeni niliowaorodhedha bali ni wadau kwa maslahi ya Taifa wanapoamua kuweka maslahi ya nchi mbele badala ya maslahi binafsi, wanakuwa tu si sehemu ya suluhisho bali ni mustakabali wa kudumu kwa amani ya taifa letu.”

Pia, Kihongosi amesema, falsafa ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya 4R ambayo ni maridhiano, Ustahimilivu, mageuzi na ujenzi upya imefungua dirisha la historia ambalo halipaswi kupuuzwa.