Na Mwandishi Wetu, Kibiti
WAZIRI wa Afya Mohamed Mchengerwa amesema boti Saba zenye thamani ya sh bilioni 1.1 zilizopatikana kwa ufafhili wa Shirika Gavi zitasaidia kuimarisha huduma za chanjo maeneo ya visiwani .
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi boti hizo iliyofanyika Bandari ya Nyamisati Kibiti Mchengerwa amesema boti hizo zitaimarisha huduma za chanjo maeneo ya visiwani yaliyopo nchini.
Amewasihu watoa huduma kuzingatia kikamilifu matakwa ya kiusalama kwa kubeba abiria wanaostahili ili kuepusha maafa
“Leo hatujakusanyika hapa kwa ajili ya kuzindua vyombo vya usafiri pekee tumekusanyika kuthibitisha falsafa kubwa ya taifa letu kwamba haki ya afya haipaswi kusimama ukingoni mwa bahari, mto, kisiwa, mwambao au umbali. Pale alipo Mtanzania, ndipo wajibu wa Serikali unapoanza. Sehemu alaiyepo mtoto anayehitaji chanjo, ndipo dhamira yetu ya huduma inapopimwa,” amesema
Mchengerwa amelishukuru Shirika Gavi kwa ufadhili boti hizo na kusema kuwa huu si msaada wa kawaida; ni uwekezaji katika uhai, kinga na usawa.

Ameongeza kuwa boti hizo zitatumika kuimarisha huduma za chanjo, hususan katika usambazaji, usimamizi shirikishi, na utoaji wa huduma za mkoba na tembezi katika maeneo ya visiwa na mwambao.
” Ndugu Wananchi, katika fikra za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, maendeleo ya kweli hayawezi kuwa neno la jukwaani pekee. Maendeleo lazima yawe na uso wa mwanadamu. Lazima yaonekane katika mama anayefikiwa na huduma, katika mtoto anayepata chanjo kwa wakati, na katika jamii ya kisiwa ambayo haisahauliki kwa sababu iko mbali na barabara kuu,” amesema Mchengerwa
Amesema mwalimu alitufundisha kwa maisha yake kwamba taifa halijengwi kwa kumuacha mtu wa mwisho nyuma. Taifa ni kama mnyororo: uimara wake haupimwi kwa kiungo kilicho katikati, bali kwa kiungo kilicho dhaifu zaidi, katika afya ya umma, mtoto mmoja asiyefikiwa na chanjo si takwimu ndogo; ni swali kubwa kwa dhamira yetu ya haki, utu na usalama wa Taifa.
Amekiri kwamba Tanzania kama nchi bado ina changamoto mbalimbali za kijiografia ambazo kwa namna moja au nyingine zinaathiri utoaji wa huduma za chanjo. Maeneo ya visiwa na mwambao mara nyingi hukumbwa na changamoto za usafiri, umbali, majira, gharama na wakati.
Matokeo yake, baadhi ya walengwa wanaweza kutofikiwa kwa wakati, jambo linaloweza kuathiri ubora wa huduma za chanjo na kinga dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.”Hii ni changamoto ya kiafya, lakini pia ni changamoto ya kifalsafa na kiutawala. Maana yake ni hii: kama jiografia inaweza kumzuia mtoto kupata chanjo, basi mkakati wa Serikali lazima uje kuvuka jiografia hiyo. Kama maji yanatenganisha ardhi, basi Serikali lazima ijenge daraja linaloelea.
Boti hizi saba ni sehemu ya daraja hilo,” amesema MchengerwaAmeongeza kuwa chanjo ina mantiki rahisi lakini nzito sana: tunamkinga mtoto leo ili Taifa lisitibu janga kesho. Ni kama mkulima anayechagua mbegu bora kabla ya mvua; asiposubiri shamba liharibike ndipo aanze kutafuta suluhisho.
Ni kama mwenye nyumba anayeziba ufa mdogo ukutani kabla ufa huo haujawa mpasuko unaoporomosha nyumba nzima. Kinga ni hekima ya kutenda mapema.” Magonjwa yanayozuilika kwa chanjo hayaheshimu mipaka ya kijiji, kata, wilaya, kisiwa au mkoa. Tukimwacha mtoto mmoja bila kinga kwa sababu anaishi mbali, hatumwachi yeye peke yake; tunaliacha Taifa katika udhaifu. Ndiyo maana uwekezaji huu wa boti saba ni jibu la kimkakati katika kulinda afya ya wananchi wetu na kuzuia milipuko ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo,” amesema
Mchengerwa ameutaja uwekezaji huu kuwa una thamani ya kiasi cha Sh 1,184,312,500 na kwamba thamani hii haipimwi kwa fedha pekee. Badala yake inapimwa kwa idadi ya watoto watakaofikiwa, familia zitakazolindwa, watumishi wa afya watakaowezeshwa, na jamii za visiwa na mwambao zitakazohisi kwamba zimo ndani ya moyo wa Taifa.
Amesema uwekezaji huu unaendana kikamilifu na juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha huduma za afya, ikiwemo utoaji wa huduma za chanjo. Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba huduma za afya hazibaki kuwa ahadi, bali zinakuwa huduma halisi zinazomfikia mwananchi kwa wakati, kwa ubora na kwa usawa.
“Kwa lugha ya kimkakati, boti hizi zinatusaidia kufanya mambo manne muhimu. Kwanza, zinapanua wigo wa kufikia walengwa. Pili, zinaongeza uhakika wa usambazaji wa chanjo na vifaa vinavyohitajika. Tatu, zinaimarisha usimamizi shirikishi wa huduma katika maeneo yenye changamoto. Nne, zinaongeza uwezo wa kutoa huduma za mkoba na tembezi kwa wakati. Huu ndio msingi wa mfumo wa afya unaomfuata mwananchi, si mwananchi kuteseka kutafuta mfumo,” amesema Mchengerwa
Amesema boti hizo zimetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa inayozingatia ubora na usalama wa vyombo vya majini. Kila boti ina vifaa vya kujiokolea, yaani life jacket, nane (8), pamoja na injini mbili zenye ukubwa wa Horsepower 100 kila moja. Hii ina maana ya uwezo mkubwa wa mwendo, uimara na uhakika zaidi katika kuwafikisha watoa huduma kwenye maeneo yanayohitaji huduma.
” Tusisahau: teknolojia bila nidhamu huwa si ukombozi kamili. Chombo kizuri bila matumizi sahihi kinaweza kupoteza maana yake. Ndiyo maana natoa rai kwa watumiaji wa boti hizi kuzingatia kikamilifu matakwa ya kiusalama, ikiwa ni pamoja na kubeba abiria wasiozidi wanane (8) kulingana na uwezo wa boti, kutumia vifaa vya kujiokolea, na kuhakikisha kila safari inazingatia taratibu zote za usalama majini,” amesema
MchengerwaAmeyataja maenro yatakayonufaika na boti hizo kwa sasa kuwa ni pamoja na Nyamisati Kibiti, Kigoma DC , Muleba, Uvinza na Zanzibar na kwanba lengo ni kuhakikksha maeneo yote ya visiwa yanapata boti kwa ajili ya kuimarisha huduma hizo

More Stories
Watumishi MZRH wang’ara maadhimisho Mei Mosi
Baobab wakutana na NBAA wapatiwa elimu ya Uhasibu
NMB yatwaa tuzo tano za Kitaifa za AOSH kwa mwaka wa Pili mfululizo