May 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi MZRH wang’ara maadhimisho Mei Mosi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KATIKA kuadhimisha siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) mwaka 2026, Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH) imewatunuku vyeti na zawadi watumishi wake waliofanya vizuri zaidi, hatua inayolenga kuongeza motisha na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa nyanda za Juu Kusini.

Akizungumza katika hafla hiyo, iliyofanyika hospitalini hapo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt. Lazaro Mboma, amesema kuwa tuzo hizo ni sehemu ya kuthamini juhudi za watumishi wanaotekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kujituma.

“Tuzo hizi ni chachu ya kuongeza juhudi, tunatambua utumishi wenu uliotukuka na tunatarajia kuona mabadiliko makubwa zaidi katika utendaji kazi ili kuifikia azma ya serikali ya kutoa huduma bora za afya,” amesema Dkt. Mboma.

Amesema kuwa ufanisi wa hospitali unategemea kwa kiasi kikubwa nidhamu, weledi na moyo wa kujitolea wa watumishi wake, akisisitiza kuwa utambuzi huo utasaidia kuongeza ari ya kazi kwa wengine.

Kwa upande wao, baadhi ya watumishi waliotunukiwa vyeti wameshukuru uongozi wa hospitali kwa kutambua mchango wao, wakiahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya taaluma zao.

Hafla hiyo pia imehudhuriwa na wawakilishi kutoka Chama cha Madaktari na Wafamasia (TMDPWU), ambao wametoa wito kwa watumishi kuendelea kulinda haki zao huku wakizingatia utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa.

Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mwaka 2026 yamefanyika kitaifa mkoani Njombe, yakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050,” huku mgeni rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na kulinda maslahi ya wafanyakazi nchini.

Kwa mujibu wa taarifa za sekta ya afya nchini, zaidi ya asilimia 70 ya huduma za afya katika hospitali za rufaa hutegemea moja kwa moja juhudi za rasilimali watu, hali inayoonesha umuhimu wa kuwatambua na kuwahamasisha watumishi ili kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.