April 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwandishi: Ismail Mayumba

Kumekuwa na ongezeko la vitendo vya udhalilishaji, uonevu wa mtandaoni (cyberbullying), pamoja na matumizi mabaya ya maudhui binafsi kama picha na video bila idhini ya mhusika. Watu wengi hufanya vitendo hivi kwa lengo la kujiongezea umaarufu mtandaoni kupata likes, maoni (comments), na wafuasi (followers).

Lakini kile kinachoonekana kama “burudani” au “maudhui ya kuvutia” kwa upande mmoja, huwa chanzo cha maumivu makubwa kwa upande wa mwingine. Waathirika wa vitendo hivi hukumbwa na athari za kisaikolojia kama msongo wa mawazo, hofu, kushuka kwa kujiamini, na hata kujitenga na jamii. Wengine hufikia hatua ya kuona mitandao ya kijamii si sehemu salama tena, bali ni kama adhabu, huku wakihisi kukosa mtetezi au msaada.

Kwa kutambua changamoto hizi, serikali ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali za kisheria kulinda usalama wa raia wake mtandaoni. Miongoni mwa hatua hizo ni kuanzishwa kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, ambayo inalenga kudhibiti vitendo vya kihalifu vinavyofanyika kupitia mifumo ya kidijitali. Aidha, mwaka 2022 serikali ilianzisha Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, ambayo inalenga kulinda faragha na usalama wa taarifa za watu binafsi.

Sheria hizi zimewekwa ili kuhakikisha kuwa kila mtumiaji wa mtandao anakuwa salama, na pia kutoa mwongozo wa nini cha kufanya pale haki zako zinapokiukwa. Ikiwa mtu atatumia vibaya taarifa zako binafsi au kukudhalilisha mtandaoni, una haki ya kuchukua hatua za kisheria, na katika baadhi ya matukio unaweza kudai fidia kwa madhara uliyopata.

Hata hivyo, changamoto kubwa ipo kwa baadhi ya Watanzania kutopenda kusoma au kufuatilia taarifa muhimu. Mara nyingi watu hulalamika kuwa hakuna sheria zinazowalinda, ilhali ukweli ni kwamba hawajachukua muda kuzitafuta na kuzisoma. Kupitia https://www.mawasiliano.go.tz/documents/cybersecurity , kuna rasilimali nyingi zinazopatikana mtandaoni zinazoelezea kwa kina sheria hizi na namna ya kuzitumia.

Ni muhimu kwa kila mtumiaji wa mtandao kujielimisha kuhusu haki zake. Elimu hii itakusaidia kutambua pale unapodhulumiwa, kuchukua hatua sahihi, na kujilinda dhidi ya madhara ya kidijitali. Badala ya kukata tamaa au kuhuzunika unapokumbana na uonevu mtandaoni, unaweza kutumia sheria hizi kama nyenzo ya kujitetea, kudai haki yako, na hata kupata fidia stahiki.

Kwa hiyo, usiwe mtumiaji wa mtandao asiye na taarifa. Jifunze, elewa, na tumia haki zako ipasavyo kwa sababu usalama wako mtandaoni unaanza na wewe mwenyewe.