July 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TTCL yatwaa Tuzo na kutoa gawio Serikalini

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeandika historia mpya baada ya kutunukiwa Tuzo Maalum na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia mafanikio makubwa ya kurejea kwenye faida na kuanza kutoa gawio kwa Serikali baada ya miaka ya changamoto za kifedha.

Katika mwaka wa fedha uliopita, TTCL ilipata faida ya Shilingi bilioni 22.9 na kutoa gawio la Shilingi bilioni 1.6 kwa Serikali, hatua iliyoliwezesha Shirika hilo kutambuliwa katika Hafla ya Tuzo za Utendaji Bora wa Taasisi za Umma iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, amesema TTCL imefanya mageuzi makubwa ya kiutendaji yaliyowezesha kubadili hasara ya Shilingi bilioni 18 iliyorekodiwa mwaka uliopita na kufikia faida ya Shilingi bilioni 22.9 mwaka huu wa fedha.

Amesema mafanikio hayo yanaonesha kuwa uwekezaji wa Serikali katika mashirika ya umma unaendelea kuzaa matunda kupitia usimamizi madhubuti, uwajibikaji na utekelezaji wa mikakati ya biashara yenye matokeo.

“Mafanikio haya yameiwezesha TTCL kutoa gawio la Shilingi bilioni 1.6 kwa Serikali, jambo linalothibitisha kuwa mageuzi yanayofanyika katika taasisi za umma yana mchango mkubwa katika kuongeza mapato ya Serikali na kukuza uchumi wa Taifa,”amesema Mchechu.

Ameongeza kuwa ongezeko la gawio kutoka kwa taasisi za umma linaakisi mafanikio ya maboresho ya kiutendaji yanayoendelea kutekelezwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, huku taasisi hizo zikiendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akikabidhi tuzo hiyo, Rais Samia ameipongeza TTCL kwa hatua kubwa iliyofikia ya kurejea kwenye faida na kuanza kuchangia mapato ya Serikali kupitia gawio.

Amesema mafanikio hayo ni ushahidi wa kuimarika kwa uongozi, usimamizi wa rasilimali na ufanisi wa shughuli za Shirika, huku akizitaka taasisi nyingine za umma kuiga mfano huo kwa kuwekeza zaidi katika teknolojia, ubunifu na mifumo ya kisasa ya usimamizi.

“Taasisi za umma zinapaswa kuongeza tija, ushindani na mchango wake katika uchumi wa Taifa kwa kuzingatia uwajibikaji, matumizi bora ya rasilimali na utendaji unaolenga matokeo,” alisema Rais Samia.

Kwa mujibu wa TTCL, mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa mageuzi ya kimkakati yaliyolenga kuimarisha biashara, kuongeza ufanisi wa huduma, kuboresha usimamizi wa rasilimali na kuwekeza katika teknolojia za kisasa za mawasiliano.

Kutunukiwa Tuzo Maalum na Mkuu wa Nchi kunatajwa kuwa uthibitisho wa hatua kubwa iliyopigwa na TTCL katika safari ya mabadiliko na kurejesha imani ya Shirika hilo kama mtoa huduma muhimu wa mawasiliano nchini.

Kurejea kwenye faida, kutoa gawio kwa Serikali na kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi kunaiweka TTCL miongoni mwa taasisi za umma zinazodhihirisha matokeo halisi ya mageuzi ya kiutendaji na thamani ya uwekezaji wa Serikali katika kukuza uchumi wa Tanzania.

Mafanikio hayo yanaendana na kaulimbiu ya mwaka huu ya “Uwekezaji Wenye Matokeo ni Nguvu ya Uchumi Shindani na Maendeleo Endelevu kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” huku TTCL ikitajwa kuwa mfano wa jinsi taasisi za umma zinavyoweza kubadilika na kuwa chachu ya maendeleo ya Taifa.